Kenya yaakhirisha kufungua tena mpaka wake na Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i99580-kenya_yaakhirisha_kufungua_tena_mpaka_wake_na_somalia
Kenya jana ilitangaza kuwa imeakhirisha kufungua tena mpaka wake na Somalia baada ya mashambulizi ya karibuni katika ardhi yake. Kundi la wanamgambo wa al Shabab lenye makao yake Somalia linatuhumiwa kuhusika na mashambulizi hayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 06, 2023 01:02 UTC
  • Kenya yaakhirisha kufungua tena mpaka wake na Somalia

Kenya jana ilitangaza kuwa imeakhirisha kufungua tena mpaka wake na Somalia baada ya mashambulizi ya karibuni katika ardhi yake. Kundi la wanamgambo wa al Shabab lenye makao yake Somalia linatuhumiwa kuhusika na mashambulizi hayo.

Wizara ya Usalama wa Ndani wa Kenya, Kithure Kindiki, ametangaza kuwa hatua ya kufunguliwa upya vituo vya mpakani vya Mandera, Lamu na Garissa haitafanyika kama ilivyotangazwa mwezi Mei mwaka huu. 

Hatua hiyo imefuatia vifo vya raia watano na maafisa wanane wa polisi katika hujuma tofauti zilizofanyika karibu na mpaka huo baina ya Kenya na Somalia mwezi uliopita; mashambulizi yanayohusishwa na kundi la Shabab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda. 

Wizara ya Usalama wa Ndani wa Kenya ameongeza kuwa, serikali itaakhirisha kufunguliwa tena vituo vya mpakani kati ya Kenya na Somalia hadi hapo  watakaposhughulikia kwa ukamilifu msururu wa mashambulizi ya kigaidi na uhalifu wa kuvuka mipaka. Kindiki amebainisha haya  alipotembelea kambi ya wakimbizi ya Daadab huko mashariki mwa Kenya karibu na Somalia. 

Mpaka wa nchi mbili hizo ulifungwa rasmi mwezi Oktoba mwaka 2011 kufuatia mashambulizi ya wanamgambo wa al Shabab ambao wamekuwa wakifanya hujuma dhidi ya serikali kuu ya Mogadishu kwa zaidi ya miaka 15 sasa.