Jeshi la Sudan lakataa kushiriki mkutano wa IGAD nchini Ethiopia
Jeshi la Sudan limekataa kushiriki mkutano wa ngazi ya juu wa kuzindua mchakato wa amani wa nchi hiyo uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia; huku mapigano yakishtadi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) wenye lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Sudan ulifanyika jana Jumatatu huko Ethiopia, ambapo mbali na Kenya, Sudan Kusini, Ethiopia na Djibouti pia ni sehemu ya mkutano huo wa amani.
Jeshi la Sudan hata hivyo limekataa kushiriki mkutano huo unaolenga kujadili jinsi ya kukomesha uhasama kati ya pande mbili zinazozozana huko Sudan, na kuwezesha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu.
Viongozi wa IGAD wamesema kwa sasa wataendelea na mpango unaoongozwa na Kenya kujaribu kupata suluhisho la mzozo unaoendelea nchini Sudan, licha ya upinzani wa utawala wa kijeshi mjini Khartoum wa mapendekezo yao.
Jenerali wa Jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan alipinga uenyekiti wa Rais William Ruto wa Kenya kwenye mchakato huo, akisema kuwa Kenya inawaunga mkono na inaendelea kuwahifadhi viongozi wa waasi wa Vikosi vya Radiamali ya Haraka (RSF).
Si Jenerali Al-Burah wala naibu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Dagalo anayeongoza RSF ameshiriki mkutano huo wa Addis Ababa, ingawaje vikosi vya RSF vimetuma wawakilishi kwenye mkutano huo wa pande kadhaa.
Zaidi ya watu 1,300 wameuawa nchini Sudan na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika mapigano ya jeshi na vikosi vya RSF yaliyoanza tokea Aprili 15. Raia wengine karibu milioni tatu wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na machafuko hayo.