UN: Vita nchini Sudan vimepelekea watu zaidi ya milioni tatu kuwa wakimbizi
(last modified Thu, 13 Jul 2023 07:58:21 GMT )
Jul 13, 2023 07:58 UTC
  • UN: Vita nchini Sudan vimepelekea watu zaidi ya milioni tatu kuwa wakimbizi

Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa vita vya karibu miezi mitatu huko Sudan vimepelekea watu zaidi ya milioni tatu kuwa wakimbizi na kutoa wito kwa pande zinazopigana kuwajibika.

Mapigano yalizuka katika nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika tangu katikati ya mwezi Aprili mwaka huu baada ya kuzuka hitilafu kati ya mkuu wa jeshi la nchi hiyo Jenerali Abdel Fattah al Burhan na aliyekuwa naibu wake Mohamed Hamdan Dagalo. Hitilafu hizo hatimaye ziliibua mapigano kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya usaidizi wa haraka (RSF).  

Safa Msehli msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) mjini Geneva Uswisi amesema kuwa watu zaidi ya milioni tatu wamekimbia nyumba zao kwa sababu ya vita vinavyoendelea huko Sudan. 

Watu milioni tatu wamekuwa wakimbizi kufuatia vita huko Sudan 

Takwimu za IOM zinaonyesha kuwa watu zaidi ya milioni 2.4 wamekuwa wakimbizi huko Sudan, huku wengine karibu ya 724,000 wamevuka mpaka na kukimbilia katika nchi jirani. Msehli amezitolea wito pande hasimu huko Sudan kusitisha mapigano. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limesema kuwa linahitaji msaada endelevu wa jamii ya kimataifa ili kutoa misaada na kuwalinda raia walioathiriwa na mapigano."

Mashuhuda wanasema kuwa mamilioni ya wakazi wa mji mkuu wa Sudan, Khartoum wamekuwa wakitaabika na ukosefu wa maji na huduma ya umeme; ambapo jana Jumatano mji mkuu huo ulikabiliwa na mashambulizi ya anga. Ndege za kivita zimekuwa zikifanya mashambulizi katika kambi mbalimbali za vikosi vya RSF tokea asubuhi ya jana. 

 

Tags