Abbas Araghchi: Wakaguzi wa IAEA wanaingia nchini kwa uamuzi wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuingia nchini kwa wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA ni uamuzi uliochukuliwa na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa kwa ajili ya kuchunguza suala la kubadilishwa mafuta ya kiwanda cha kuzalisha umeme cha Bushehr. Amesema hakuna maafikiano yoyote yaliyofikiwa kuhusu ushirikiano mpya wa Iran na wakala huo.
Seyyed Abbas Araghchi amesema katika mahojiano Jumatano, akiashiria matamshi ya maafisa wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuhusu kuwasili nchini kwa wakaguzi wa wakala huo na kusema kwamba sheria iliyopitishwa Bungeni iliweka wazi ushirikiano wa baadaye wa wakala huo mikononi mwa Baraza Kuu la Usalama la Taifa, kwa hivyo, kwa mujibu wa sheria hiyo, maombi yote ya ushirikiano ya IAEA yanaelekezwa moja kwa moja katika Baraza Kuu la Usalama la Taifa kwa ajili ya kuchukuliwa maamuzi ya mwisho. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameongeza kuwa: "Maamuzi yamefanywa kuhusu ubadilishaji wa mafuta ya kiwanda cha kuzalisha umeme cha Bushehr, jambo ambalo linapasa kufanywa chini ya usimamizi wa wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, na ushirikiano wa aina yoyote katika uwanja huo utafanyika katika fremu ya sheria hiyo ya Bunge, ambayo itahudumia maslahi ya taifa la Iran."