Kumalizika muda wa vikwazo vya makombora dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i103660-kumalizika_muda_wa_vikwazo_vya_makombora_dhidi_ya_iran
Tarehe 18 Oktoba 2023 vikwazo vya makombora dhidi ya Iran vilimalizika kwa mujibu wa Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Baada ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kutangazwa Juni 2015, iliamuliwa kuwa vikwazo vya silaha vya Iran vitamalizika baada ya miaka 5, yaani Oktoba 2020, na vikwazo vya makombora vitamalizika baada ya miaka 8 yaani Oktoba 2023.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 19, 2023 01:09 UTC
  • Kumalizika muda wa vikwazo vya makombora dhidi ya Iran

Tarehe 18 Oktoba 2023 vikwazo vya makombora dhidi ya Iran vilimalizika kwa mujibu wa Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Baada ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kutangazwa Juni 2015, iliamuliwa kuwa vikwazo vya silaha vya Iran vitamalizika baada ya miaka 5, yaani Oktoba 2020, na vikwazo vya makombora vitamalizika baada ya miaka 8 yaani Oktoba 2023.

Kimsingi, silaha za makombora za Iran ni za kujilinda na majaribio ya makombora ya Iran pia yanafanyika ili kuboresha uwezo wake wa makombora ya balestiki. Kwa kutilia mkazo kuwa sera zake zimeegemezwa kwenye msingi wa kujilinda na kujihami, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza juu ya haki yake ya kuboresha mpango wake wa makombora kwa ajili ya kujilinda.

Iran inategemea wataalamu wake wa ndani na uwezo wake katika uga wa kupanua na kuboresha makombora yake, na siasa za vikwazo za Marekani na washirika wake wa Magharibi, za kuizuia isijiimarishe katika uwanja wa makombora au kuizuia isipate zana zinazohitajika katika uwanja huo hazijaweza kuwa na taathira kubwa katika kuzuia kuboreshwa mfumo wa makombora ya Iran. Iran sasa ni mojawapo ya mataifa yenye uwezo mkubwa wa makombora duniani.

Vladimir Sagin, mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi, anasema: Tehran ilijibu vikwazo vya Marekani kwa kuimarisha mpango wake wa makombora, na juhudi za Marekani za kusimamisha mpango huo hazijakuwa na mafanikio yoyote.

Makao makuu ya Umoja wa Ulaya

Marekani, ikiwa na waitifaki wake wa Ulaya, ambao  wanataka kuhodhi teknolojia ya hali ya juu, daima wamekuwa wakiizuia Iran kujiendeleza katika nfumo wa makombora. Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya (Ujerumani, Ufaransa na Uingereza), ambazo ni wanachama wa kundi la 4+1, na Marekani, daima zimekuwa na mtazamo hasi kuhusu silaha na uwezo wa makombora wa Iran na kuzitaja juhudi zake katika uwanja huo kuwa kinyume cha sheria. Moja ya matakwa makuu ya Marekani, ambayo Wazungu pia wamekubaliana nayo  ni kusimamisha mpango wa makombora wa Iran.

Licha ya madai ya Ulaya ya kuunga mkono makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini umoja huo umechukua msimamo kama wa Marekani kuhusiana na makombora ya Iran.

Kuhusiana na suala hilo, Baraza la Ulaya lilitangaza katika taarifa yake Jumanne, Oktoba 17 kwamba nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zitaendeleza vikwazo vya awali vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran katika uga wa silaha na makombora, hata baada ya kumalizika muda wake tarehe 18 Oktoba. Kwa mujibu wa Baraza la Ulaya, vikwazo hivyo dhidi ya Iran si vipya, na havibadilishi vikwazo vya hapo awali vya Umoja wa Ulaya kuhusiana na  makubaliano ya nyuklia. Awali Troika ya Ulaya ilidai kwamba itadumisha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran kutokana na kile ilichodai Iran kutotekeleza wajibu wake katika makubaliano ya nyuklia. Vikwazo hivyo vilizuia  Iran kutengeneza makombora ya balestiki yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia, pamoja na kununuliwa ndege zisizo na rubani na makombora kutoka Iran au kuiuzia Iran silaha hizo. Hata hivyo, vikwazo hivyo hivi sasa vimemalizika leo  tarehe 18 Oktoba, kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA.

Nasser Kanani Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Katika radiamali yake kuhusiana na uamuzi wa Jumuia ya Umoja wa Ulaya wa kutoketekeza ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano hayo  Nasser Kanani, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema siasa za Umoja wa Ulaya zinakwenda kinyume na makubaliano ya umoja huo pamoja na nchi tatu za Ulaya na zinaonyesha wazi nia yao mbaya kuhusiana na jambo hilo.

Hivi sasa, baada ya kumalizika vikwazo vya silaha na makombora dhidi ya Iran, Tehran inaweza kuchukua hatua mbalimbali katika uga wa silaha na utengenezaji wa makombora, na wakati huo huo haitakuwa na vizuizi vyovyote vya kuagiza na kuuza nje silaha zake.