Feb 19, 2024 04:33 UTC
  • Kuzinduliwa mifumo mipya ya makombora nchini Iran

Katika kuendelea ustawi wa Jamhuri ya Kiislamu katika sekta ya makombora, mifumo dhidi ya makombora ya balestiki kwa jina la "Arman", na mfumo wa ulinzi wa anga ya juu wa Azarkhash, ambao uliundwa kwa juhudi za wataalamu wa Wizara ya Ulinzi ya Iran ulizinduliwa juzi Jumamosi.

Baada ya kutayarishwa, mifumo hii ya kutungua makombora inaweza kulenga na kuharibu shabaha husika katika muda wa chini ya dakika 3. Uwezo wa ulinzi wa anga wa Jamhuri ya Kiislamu utaongezeka kwa kiasi kikubwa kwa kuwepo mifumo hii mipya  ya kukabiliana na makombora katika mtandao wa ulinzi wa Iran.  

Makombora yaliyotumiwa katika mifumo ya kutungua makombora ya balestiki kwa jina la "Arman" wa aina ya Sayad-3 yana uwezo wa kukabiliana kwa wakati mmoja dhidi ya shabaha 6 katika umbali wa kilomita 120 hadi 180. Mfumo wa Azarakhsh ni mfumo wa kuwekwa kwenye majabari na wa masafa mafupi ambao kwa wakati mmoja hutumia rada na mfumo wa macho ya elektro-optiki  kwa ajili ya kutambua na kufuatilia shabaha.

Mfumo mpya wa makombora ya Iran

Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa mifumo mipya ya kutungua makombora katika mtandao wa ulinzi wa anga wa nchi, Brigedia Jenerali Amir Ashtiani Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema wizara yake imeelekeza nguvu zake zote katika kukidhi mahitaji ya uwanja wa ulinzi, zana na silaha za vikosi vya jeshi sambamba na uwezo wa ulinzi na muendelezo wa uzinduzi wa yaliyoahidiwa.

Wiki iliyopita, kwa mara ya kwanza, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilifanikiwa kurusha makombora ya balestiki yenye uwezo wa kuruka umbali wa kilomita 1,700 kutoka katika meli ya kivita ya kikosi ch ulinzi kuelekea shabaha zilizowekwa. Mafanikio haya mapya yanamaanisha kuwa ushawishi na nguvu za kijeshi za majini na za makombora za Iran zitaongezeka na kufika hadi sehemu yoyote duniani kwa ajili ya kudhamini usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Maendeleo ya Iran katika sekta za makombora, mifumo ya ulinzi wa angani na ndege zisizo na rubani (droni) daima yamekuwa mwiba kwa maadui wa mfumo wa Kiislamu katika miaka ya hivi karibuni. Kuhusiana na nukta hii, kumekuwepo na utendaji kazi wa karibu na ushirikiano mkubwa kati Wizara ya Ulinzi ya Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC); na jambo hilo lina nafasi muhimu katika maendeleo ya sekta tajwa.

Brigedia Jenerali Amir Ashtiani Waziri wa Ulinzi wa Iran

Hii ni katika hali ambayo  baada ya vita vya miaka 8 vya kulazimishwa vya Iraq dhidi, maadui wa taifa la Iran mara kwa mara wamekuwa wakipanga njama tata zenye nia ya kuivamia Iran ya Kiislamu, lakini kutokana na kuwa macho Jeshi la Iran (Artesh) na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC au SEPAH) maadui hawathubutu kuivamia Iran.

Ikumbukwe kuwa, Iran ina nafasi muhimu ya kistratijia na kijiografia katika eneo la Magharibi mwa Asia, na kwa ajili hiyo, mfumo wa ubeberu na uistikbari wa kimataifa daima unalitazama eneo hili la kijiografia kwa macho ya pupa katika muda wote wa historia. Kwa msingi huo, hakuna shaka yoyote kuwa ulinzi wa Iran ya Kiislamu kama Imam Khomeini (RA) alivyosema, ni moja ya "wajibu" na ishara ya nguvu ya vikosi vya kijeshi vya Iran.

Kombora la balestiki la Mahdavi likivurumishwa kutoka meli ya kivita ya Iran ya Shahid

Kwa hakika, umuhimu wa nguvu uko katika uwezo wa kujihami na kumfanya adui asithubutu kuanzisha vita na migogoro yoyote. Ingawa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kuanzisha vita, lakini uzoefu wa miaka minane ya vita vya kulazimishwa umethibitisha kwamba iwapo itatishwa na kushambuliwa  basi italinda usalama wake kwa nguvu na uwezo wake wote.

Suala jengine ambalo limepelekea kuimarishwa nguvu ya kiulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  ni uwepo wa kijeshi wa madola ajinabi yanayoingilia mambo ya ndani ya eneo kwa lengo la kuziuzia silaha baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi.

Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zinapinga kuimarishwa kwa ulinzi na uwezo wa makombora wa Iran na kuutaja kuwa ni tishio kwa usalama wa eneo hili ili kuligeuza eneo hilo kuwa ghala la kuhifadhia silaha zake.

 

Tags