Mar 03, 2024 07:40 UTC
  • Raisi: Iran ipo tayari kuipa Msumbiji uzoefu wa kiufundi na kiuhandisi

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ina hamu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano na mataifa ya Afrika ikiwemo Msumbiji na kuongeza kuwa, kuna haja ya kubuni ramani mpya ya njia na kuamilisha Kamisheni ya Pamoja ya Iran na Msumbiji ili kupiga jeki ushirikiano wa pande mbili.

Sayyid Raisi amesema hayo katika mkutano wake na Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji, pambizoni mwa Mkutano wa Saba wa Wakuu wa Nchi Zinazouza Gesi Duniani (GECF) nchini Algeria na kuongeza kuwa, Iran ipo tayari kuipa Msumbiji huduma za kiufundi na kiuhandisi.

"Mkutano huu unaweza kufungua ukurasa mpya katika muelekeo wa kuimarisha na kuboresha ushirikiano baina ya nchi mbili," ameeleza Rais Raisi.

Rais wa Iran amebainisha kuwa, utawala wa Kizayuni na nchi za Magharibi kwa kuunga mkono ugaidi, zinaziweka nchi za Afrika chini ya mashinikizo na kupora rasilimali zao. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kushirikiana na Afrika katika vita dhidi ya ugaidi.

Kwa upande wake, Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji amesema nchi yake inatazama suala la kuimarisha uhusiano na Iran kuwa msingi wa kufikia malengo muhimu, huku akitoa mwito wa kutekelezwa makubaliano baina ya nchi mbili hizi.

Rais wa Iran na Rais Kais Saied wa Tunisia

Kabla ya kwenda Algeria, Rais Ebrahim Raisi wa Iran alieleza kuwa, Afrika ina nafasi muhimu katika sere za nje za serikali yake na akasema: "Suala la kuwa na mahusiano na Afrika kwa ujumla, hususan nchi za Kiislamu barani humo lina nafasi ya pekee sana katika sera yetu ya mambo ya nje."

Kadhalika Rais wa Iran amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Kais Saied wa Tunisia huko Algiers na kusema kuwa, Iran ipo tayari kulipa taifa hilo la Afrika uzoefu wake katika uga wa sayansi na teknolojia.

Amesema Iran na Tunisia zina mtazamo mmoja juu ya kadhia ya kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina na kuongeza kuwa, kuna haja ya kuchukuliwa hatua athirifu kulinda haki za msingi za Wapalestina.

Tags