Apr 27, 2024 13:27 UTC

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika sherehe za ufunguzi wa maonyesho ya sita ya uwezo wa mauzo ya nje ya bidhaa za Iran (Iran Expo 2024) kwamba maonesho haya yanaonyesha kuwa Iran haiwezi kuwekewa vikwazo na ina uwezo wa kufanya uvumbuzi katika nyanja mbalimbali.

Sayyid Ebrahim Raisi, ambaye mapema leo (Jumamosi) amehutubia sherehe za ufunguzi wa Maonyesho ya 6 ya Uwezo wa Kuuza Nje Bidhaa za Iran (Iran Expo 2024), amesema kuwa maonyesho haya yanajenga mazingira ya ushindani kwa ajili ya ustawi wa jamii kupitia maendeleo ya biashara, mauzo ya nje na upanuzi wa maingiliano ya kiuchumi. Amesema: Maonyesho haya yanakuza maendeleo ya kiuchumi nchini, kanda na dunia nzima.

Sayyid Raisi ameongeza kuwa: Maonyesho haya yanaonyesha baadhi ya mafanikio ya vijana wa Iran ambao wamegeuza vitisho na vikwazo kuwa fursa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekumbusha kuwa, iwapo wanadamu hawatachukua hatua za kuzinyima nchi rasilimali na kutodhulumu maumbile, ulimwengu na ubinadamu kutokana na ulafi wa watawala, suhula hizo zitapatikana kwa kila mtu na mahitaji ya mwanadamu yanaweza kukidhiwa.

Sayyid Ebrahim Raisi amevitaja vikwazo kuwa ni aina ya vita visivyo vya kijeshi vinavyolinyima taifa mahitaji yake; lakini katika vita vya azma na irada, taifa lenye irada na azma thabiti la Iran, limeweza kuvuka vikwazo hivyo, kwa kadiri kwamba msemaji wa Ikulu ya Rais wa Marekani, White House, ametangaza kwamba mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu yameshindwa kwa njia ya kufedhehesha.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa: Nguvu ya uzalishaji na mauzo ya nje ya Iran inaongezeka sambamba na nguvu zake za kijeshi.

Maonyesho ya sita ya uwezo wa kusafirisha nje bidhaa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRAN EXPO 2024) yameanza leo mjini Tehran kwa lengo la kuonesha uwezo wa kiuchumi wa Iran na yataendelea hadi tarehe Mosi Mei.

Tags