Watu 7 wafariki dunia katika janga la mafuriko Mash'had, Iran
Mvua kubwa iliyonyesha Mashhad, jiji la pili kwa idadi kubwa ya watu nchini Irani, imesababisha vifo vya watu saba na 12 kutoweka.
Mkuu wa Kitengo cha Zimamoto cha Manispaa ya mji wa Mash'had, Hamidreza Kafiniya amesema kuwa, watu saba walifariki katika mafuriko yaliyosababishwa na mvua kuubwa hapo jana, wakiwemo wawili walionasa ndani ya gari lililokuwa chini ya maji eneo la medani ya Mashhad Inkilap na mama mmoja na watoto wake wanne waliofariki dunia wakiwa wamenasa nyumbani kwao.
Kikosi cha zima moto kilianza kusaidia wahanga wa mafuriko hayo mchana na kuendelea na shughuli za utafutaji na uokoaji.

Muhsin Zakiriyan, Mkuu wa Hilali Nyekundu ya Khorasan Razavi, amesema watu 12 hawajulikani walipo. Gavana wa Mashhad Mohsen Daveri amesema kwa akali familia 250 katika nyumba 150 zilizoharibiwa zilihamishwa hadi maeneo tofauti ya jiji na vijiji vinavyozunguka.
Video zilizochapishwa na kusambaa katika mitandao ya kijamii zinaonyesha magari yakizamishwa na kusombwa na mkondo wa maji.
Wilaya kadhaa zimeripoti kukatika kwa umeme, huku watu wakikwama kwenye lifti.