Iran yakadhibisha madai ya Marekani kuhusu Yemen, yasema ni uongo mtupu
Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amepuuzilia mbali madai ya Marekani iliyosema Jamhuri ya Kiislamu inaingilia masuala ya Yemen na kusema kuwa, Washington inalenga kufikia maslahi yake ya kisiasa katika eneo la Magharibi mwa Asia kupitia njia ya kueneza uwongo na upotoshaji.
Amir Saeid Iravani ametoa kauli hiyo katika barua aliyoituma kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, na Rais wa zamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Pedro Comissario Afonso, akijibu tuhuma za hivi karibuni za Marekani dhidi ya Iran katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Yemen.
Wakati wa mkutano wa hadhara wa UNSC Mei 13, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Robert Wood, alidai kuwa Jamhuri ya Kiislamu inatuma "silaha za hali ya juu, yakiwemo makombora ya balistiki" kwa ajili ya jeshi la Yemen na harakati ya Muqawama ya Ansarullah.
"Inasikitisha kwamba, kwa mara nyingine tena, mwakilishi wa Marekani ametumia jukwaa la Baraza la Usalama kuendeleza maslahi yake ya kisiasa yenye muono finyu na kuhalalisha vitendo haramu na uvamizi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya mamlaka na ardhi ya Yemen kwa kueneza uwongo na habari potofu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu hali ya Yemen,” inasema sehemu ya barua hiyo ya Iravani.
Amesisitiza kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakanusha madai haya yasiyo na msingi."
Iravani pia alikanusha madai kama hayo yaliyotolewa dhidi ya Tehran na wawakilishi wa Marekani, Uingereza na Ufaransa katika mkutano mwingine kuhusu Yemen mwezi Aprili.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweka wazi kwamba Tehran inatekeleza maazimio husika ya Baraza la Usalama kuhusu hali ya Yemen na haijajihusisha na shughuli zinazokiuka maazimio hayo."
Itakumbukwa kuwa, vikosi vya jeshi vya Yemen vimefanya makumi ya operesheni za kijeshi dhidi ya meli zenye uhusiano na Israel tangu Oktoba 2023, wakati utawala huo ghasibu ulipoanzisha vita na mauaji ya kimbari yanayoungwa mkono na kufadhiliwa na nchi za Magharibi dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Kiongozi wa Ansarullah Abdul-Malik al-Houthi ametangaza kuwa vikosi vya Yemen vitalenga meli yoyote inayoelekea bandari za Israel, bila kujali inatoka wapi.
Marekani na Uingereza tangu katikati ya mwezi wa Januari zimekuwa zikifanya mashambulizi ya anga na makombora dhidi ya Yemen, na kuisaidia Israel kwa silaha, fedha na kadhalika.