Iran: Marekani na Magharibi hazisiti kukiuka sheria za kimataifa
Msemaji wa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameasema kuwa sheria za kimataifa zinakabiliwa na udhaifu wa dhamana ya utekelezaji na kusisitiza kuwa: Marekani na nchi za Magharibi kwa ujumla zinakubali sheria za kimataifa kiubaguzi na hazisiti kukanyaga haki hizo kwa kutumia visingizo vya kisiasa.
Ali Bahadori Jahromi, msemaji wa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika leo katika ukurasa wake wa mtandao wa X kwamba: Sheria za kimataifa zinakabiliwa na udhaifu wa dhamana ya utekelezaji, na baadhi ya maoni ya kisiasa pia yanaziidisha tatizo hilo. Jahromi ametolea mfano barua iliyoandiikwa na maseneta 12 wa Marekani wakitoa vitisho vya kuiadhibu na kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na majaji wake iwapo watatekeleza wajibu wao wa kisheria!
Siku chache zilizopita, barua iliyotiwa saini na maseneta 12 wa Marekani iliyotumwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilichapishwa katika vyombo vya habari, ambapo maseneta hao wa Marekani walitishia kuwawekea vikwazo majaji wa Mahakama ya kimataifa ya Junai (ICC) iwapo watatoa kibali cha kukamatwa maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Isarel waliohusika na mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gazz huko Palestina.
Msemaji wa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: Nukta inayopaswa kupewa mazingatio kuhusiana na barua hiyo ya vitisho ya maseneta wa Marekani ni kwamba, ufanisi wa mfumo wa kisheria wa kimataifa unahitaji marekebisho makubwa katika suala zima la muundo na maudhui yake.
Bahadori Jahromi pia ameandika: Mienendo ya nchi za Magharibi imepunguza kasi ya mchakato wa ukomavu wa sheria za kimataifa na utekelezaji wake.
Amesema: Moja ya mifano ya wazi ya mtazamo wa kisiasa na upendeleo wa nchi za Magharibi kuhusiana na masuala ya haki za binadamu ni hali ya hivi karibuni ya mauaji ya kimbari ya utawala wa Israel, mashambulizi dhidi ya raia, vituo vya matibabu na elimu, makao makuu ya mashirika ambayo yako chini ya himaya ya kimataifa au vituo vya habari, na vilevile mauaji ya halaiki ya watoto na wanawake wa Kipalestina huko Gaza.