Rais wa mpito: Sera ya Raisi ya kuimarisha uhusiano na Iraq itaendelea
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i112180-rais_wa_mpito_sera_ya_raisi_ya_kuimarisha_uhusiano_na_iraq_itaendelea
Rais wa mpito wa Iran Mohammad Mokhber amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendeleza kwa uthabiti sera ya hayati rais Ebrahim Raisi ya kukuza uhusiano na Iraq.
(last modified 2024-05-26T00:55:20+00:00 )
May 26, 2024 00:55 UTC
  • Rais wa mpito: Sera ya Raisi ya kuimarisha uhusiano na Iraq itaendelea

Rais wa mpito wa Iran Mohammad Mokhber amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendeleza kwa uthabiti sera ya hayati rais Ebrahim Raisi ya kukuza uhusiano na Iraq.

Mokhber aliyasema hayo Jumamosi alipokutana na Rais Abdul Latif Rashid wa Iraq na ujumbe aliofuatana nao ambao uko mjini Tehran kwa ajili ya kutoa heshima kwa Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian na wenzake waliopoteza maisha katika ajali ya helikopta wiki iliyopita.

Mokhber amesema hasara kubwa na chungu ya marehemu rais imeimarisha umoja wa kitaifa ndani ya nchi na kuunda muunganiko na maelewano kati ya muqawama na nchi za Kiislamu.

Ameongeza kuwa moja ya mafanikio makubwa ya marehemu rais ni kuboresha uhusiano wa Iran na Waislamu na nchi jirani. Rais huyo wa mpito amesisitiza kuwa, serikali na taifa la Iraq zina nafasi kubwa katika siasa za nje za Iran.

Amebainisha kuwa marehemu rais alikuwa na nafasi kubwa na yenye taathira katika kuimarisha safu ya muqawama, kubadilisha mlingano wa utawala duniani kwa kuendeleza mashirikiano na nchi huru na kuushinda utawala wa Marekani na Israel.

Amesema Iran itaendeleza msimamo wake thabiti wa kuunga mkono mapambano kwa kuzingatia miongozo ya busara ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Mashahidi Rais wa Iran Ebrahim Raeisi (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian

Rais wa Iraq kwa upande wake amepongeza uungaji mkono wa Iran kwa nchi yake na kusema kufa shahidi Rais Raisi sio tu ni janga kubwa na lisiloweza kurekebishwa kwa taifa la Iran bali pia watu wa Iraq na eneo zima. Rashid ameongeza kuwa, serikali na taifa la Iraq litasimama upande wa serikali na taifa la Iran katika tukio hilo chungu nzima.

Ameeleza azma ya Baghdad ya kuboresha zaidi uhusiano na Tehran, akisema nchi yake itachukua hatua zote zinazohitajika katika suala hili. Ziara ya Rashid mjini Tehran imekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Iraq Mohammed Shia’ al-Sudani kutembelea Tehran kukutana na Ayatullah Khamenei na kuhudhuria msafara wa mazishi ya Raisi na viongozi wengine wa nchi.

Mnamo Mei 19, helikopta iliyokuwa imembeba Raisi na wasaidizi wake ilianguka katika eneo la milima na misitu katika Mkoa wa Azarbaijan Mashariki nchini Iran. Miili yao ilipatikana siku iliyofuata baada ya msako mkali.