Ajali mbaya ya basi la shule Uganda yaua watoto 20
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139952-ajali_mbaya_ya_basi_la_shule_uganda_yaua_watoto_20
Watoto wasiopungua 20 na mtu mmoja mzima wamefariki dunia baada ya basi la shule walilokuwa wakisafiria kupata ajali katika Wilaya ya Kapchorwa, mashariki mwa Uganda, polisi wamesema.
(last modified 2026-07-17T11:42:54+00:00 )
Jul 17, 2026 11:41 UTC
  • Wanafunzi 20 wafariki dunia katika ajali ya Uganda
    Wanafunzi 20 wafariki dunia katika ajali ya Uganda

Watoto wasiopungua 20 na mtu mmoja mzima wamefariki dunia baada ya basi la shule walilokuwa wakisafiria kupata ajali katika Wilaya ya Kapchorwa, mashariki mwa Uganda, polisi wamesema.

Kwa mujibu wa Polisi wa Uganda, ajali hiyo ilitokea Alkhamisi usiku wakati basi la Shule ya Msingi ya King David Junior kutoka Kampala lilipokuwa likirejea baada ya ziara ya masomo katika maporomoko ya maji ya Sipi Falls.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa dereva alipoteza udhibiti wa basi, likatoka nje ya barabara, kugonga jiwe kubwa lililokuwa kando ya barabara na baadaye kupinduka.

Polisi wamesema manusura wakiwemo watu wazima watatu na watoto kadhaa, walikimbizwa hospitalini kwa matibabu, huku idadi kamili ya waliojeruhiwa ikiendelea kubainishwa.

Polisi wamesema basi lililohusika katika ajali hiyo lilikuwa linamilikiwa na Shule ya King David Junior, shule ya msingi iliyoko katika mji mkuu wa Uganda, Kampala.

Mamlaka zimeanzisha uchunguzi ili kubaini chanzo kamili cha ajali hiyo, ambayo ni miongoni mwa ajali mbaya zaidi za usafiri wa wanafunzi nchini Uganda katika kipindi cha hivi karibuni. Aidha, ajali za mabasi na malori zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara nchini humo kutokana na changamoto za usalama barabarani na hali ya baadhi ya barabara.

Mwezi Oktoba mwaka uliopita (2025), abiria 46 walipoteza maisha yao katika ajali nyingine ya barabarani katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki ambayo hupoteza watu karibu elfu tano kila mwaka.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Polisi wa Uganda ya mwaka 2024, watu 5,144 walifariki dunia katika ajali za barabarani mwaka 2024, sawa na wastani wa vifo 14 kila siku. Idadi hiyo iliongezeka kwa asilimia 7 ikilinganishwa na watu 4,806 waliokufa mwaka 2023, ambao walikuwa wastani wa vifo 13 kwa siku.