Jun 19, 2024 11:32 UTC
  • Waziri Owji: US haina ubavu wa kuzuia uuzaji wa mafuta ya Iran nje ya nchi

Waziri wa Mafuta wa Iran amesema kuwa, hakuna serikali yoyote ya Marekani yenye uwezo na ujasiri wa kuzuia uuzaji wa mafuta ya Jamhuri ya Kiislamu nje ya nchi.

Javad Owji amesema hayo leo Jumatano akiwasilisha ripoti ya mauzo ya mafuta na gesi ya Iran katika kikao cha wazi cha Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na kuongeza kuwa, mauzo ya mafuta ya Iran nje ya nchi yameongezeka kwa kiasi kikubwa licha ya vikwazo vya Marekani.

Amesema licha ya vikwazo vipya 600 dhidi ya uuzaji nje wa mafuta na bidhaa za petrokemikali za Iran, lakini Jamhuri ya Kiislamu imeongeza uzalishaji wa mafuta kwa mapipa milioni 1.4 kwa siku, katika muda wa miaka mitatu iliyopita.

Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza bayana kuwa, Tehran itaendelea kuongeza uzalishaji na usafirishaji wa mafuta hadi kufikia kiwango chake cha kabla ya kuwekewa vikwazo.

Mhandisi Owji ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu hivi sasa inajitosheleza kikamilifu katika sekta ya uchimbaji mafuta na gesi, baharini na katika nchi kavu, licha ya kuwa chini ya mashinikizo na vikwazo vya maadui.

Waziri huyo ameliambia Bunge la Iran kuwa, "Kwa hatua zilizochukuliwa na serikali katika sekta ya mafuta na maandalizi kambambe katika uga wa uuzaji wa bidhaa za mafuta na kilimo nje ya nchi, sina budi kutangaza kuwa, utawala wowote utakaochukua mamlaka Marekani hauwezi kuizuia Iran kuzalisha na kusafirisha nje mafuta yake."

Tags