Iran yapongeza makubaliano ya makundi ya Palestina ya Beijing China
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amekitaja kikao cha hivi karibuni cha makundi ya Palestina mjini Beijing China na makubaliano yaliyofikiwa kuwa ni katika mwelekeo wa mapatano na maridhiano ya kitaifa. Nasser Kan'ani Chafi amesema hiyo ni hatua yenye thamani kubwa na "harakati ya kuelekea katika mwelekeo sahihi".
Kan'ani Chafi amesisitiza kuwa, kama ilivyokuwa huko nyuma, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeazimia kuunga mkono kadhia ya taifa la Palestina na maafikiano ya makundi ya Palestina katika kukabiliana na kukaliwa kwa mabavu na utawala wa kibaguzi wa Israel na harakati zao za pamoja za kuelekea kutumia haki ya kimsingi ya kujitawala, kwa kutambua uhuru na mamlaka ya kujitawala ardhi yote ya Palestina na kuundwa kwa taifa huru la Palestina mji mkuu wake ukiwa Baytul-Muqaddas.
Makundi na mirengo mbalimbali ya Kipalestina zikiwemo Harakati za Fat'h na Hamas Jumanne iliiyopita zilitia saini taarifa mjini Beijing yenye lengo la kumaliza hitilafu na kuimarisha umoja wa Wapalestina.
Viongozi wa makundi ya Palestina wamesisitiza katika taarifa hiyo juu azma yao ya kuhitimisha mpasuko na mgawanyiko na kuimarisha umoja baina ya makundi ya Palestina.
Aprili mwaka huu, Beijing iliandaa duru ya kwanza ya mikutano kati ya viongozi wa Fat'h na Hamas ili kufikia makubaliano. Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China Lin Jian alisema mapema mwezi Aprili kwamba, wawakilishi wa Fat'h na Hamas walifanya mashauriano mjini Beijing "kuhusu kuendeleza maridhiano kati ya Wapalestina na mazungumzo ya kina na ya wazi."