Indhari ya Ali Bagheri kwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani
Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kufungwa vituo vya Kiislamu nchini Ujerumani ni kitendo cha kisiasa kabisa kinachoendana na chuki dhidi ya Uislamu na maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ali Bagheri amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Annalena Baerbock, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani na kujadiliana naye kuhusu hatua isiyo ya kisheria na inayokinzana na haki za binadamu ya polisi wa nchi hiyo ya bara Ulaya ya kufunga vituo vya Kiislamu nchini Ujerumani kikiwemo Kituo cha Kiislamu cha Hamburg.
Serikali ya Ujerumani imepiga marufuku shughuli za kituo cha Kiislamu cha Hamburg na taasisi tanzu za kituo hicho licha ya umuhimu wake mkubwa kwa Waislamu.
Kituo cha Kiislamu cha Hamburg ni miongoni mwa vituo muhimu vya Kiislamu nchini Ujerumani na barani Ulaya kwa ujumla.
Mbali na kwamba makao yake makuu yako Hamburg, lakini kituo hicho cha Kiislamu ambacho kina moja ya Misikiti ya kale zaidi nchini Ujerumani, kina matawi katika maeneo mbalimbali kama vile Frankfurt, Munich na Berlin na vituo vyote hivyo vimefungiwa hivi sasa kwa amri ya serikali ya Ujerumani.
Huku akionyesha kutoridhishwa na hatua hiyo ya vyombo vya usalama vya Ujerumani na kuilaani vikali, Bagheri amesema kuwa, kufungwa kwa vituo vya Kiislamu nchini Ujerumani ni hatua ya kisiasa na kinyume kabisa na Uislamu na serikali ya Ujerumani lazima ikubali matokeo yake.
Kuna vituo vingi vya Kiislamu nchini Ujerumani ambavyo vina historia kongwe. Kwa sababu Uislamu ni dini ya waliowachache zaidi nchini Ujerumani na Waislamu ni takriban 5.4% ya wakazi wa nchi hiyo, miongoni mwa vituo vya Kiislamu nchini Ujerumani ni Kituo cha Kiislamu cha Hamburg ambacho kina moja ya misikiti mikongwe zaidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia barani Ulaya.
Tarehe 16 mwezi huu wa Julai, polisi wa Ujerumani walifanya uvamizi katika kituo cha Kiislamu cha Hamburg na taasisi kadhaa za Kiislamu zilizoko chini ya kituo hicho yakiwemo majengo 53 katika maeneo manane tofauti ya Ujerumani kwa madai ya kufanya uchunguzi. Kituo cha Hamburg hivi sasa kinatuhumiwa na shirika la ujasusi la Ujerumani kuwa eti kinaendesha siasa kali na eti kina chuki na Mayahudi kwa kuwa kinaunga mkono Palestina na kinapinga jinai na ukatili unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Ismail Bagheri, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na suala hilo: “Muamala wa polisi wa Ujerumani dhidi ya shughuli za vituo vya Kiislamu nchini humo ulikuwa ni kwa mujibu wa hali ya kisiasa ya chuki dhidi ya Uislamu ambayo ilichochewa na makundi ya chuki dhidi ya Uislamu na duru za Kizayuni barani Ulaya.
Katika hali ambayo, serikali ya Ujerumani ilitarajiwa kusimama dhidi ya makundi hayo ya chuki dhidi ya Uislamu, imekwenda sambamba nayo, jambo ambalo huenda likawa na madhara na matokeo mabaya. Kituo cha Kiislamu cha Hamburg ambacho kimekuwa kikiendesha shughuli zake kwa takribani miongo minane, kiliasisiwa mwaka 1953 kwa himaya na uungaji mkono wa Ayatullah Boroujerdi.
Kwa miaka yote hii kituo hicho kimekuwa kikifanya shughuli zake za kidini na kiutamaduni ikiwa ni pamoja na kutoa huduma mbalimbali za kiushauri, za kimasomo n.k. Kituo hicho cha Kiislamu kina zaidi vitabu 6,000 vya maudhui tofauti. Kituo cha Kiislamu cha Hamburg kimekuwa na mchango mkubwa wa kuenea mafundisho sahihi ya Uislamu nchini Ujerumani. Hiyo ni sehemu ambayo Waislamu walikuwa wanakusanyika kwa shughuli zao mbalimbali.
Mbali na utendaji wa kidini kwa Waislamu, kituo hiki kimekuwa ni mtangazaji wa Uislamu wa kuuvumiliana katikati mwa Ulaya kwa kuanzisha mawasiliano na mdakhala na wafuasi na wanafikra wa dini nyinginezo.
Hapana shaka kuwa, kufungiwa kituo hicho muhimu cha Kiislamu, kunazidi kuonesha jinsi madola ya kibeberu yasivyo wakweli hata kidogo katika madai yao ya kupigania haki za binadamu, uhuru wa maoni na uhuru wa kuabudu, bali ni chuki na uadui dhidi ya Uislamu na Waislamu tu ndio unaotawala ndani ya tawala hizo.