Iran yatangaza kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Gambia
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Gambia zimerejesha uhusiano wao wa kidiplomasia baada ya kusimama kwa takriban miaka 14.
Kufuatia mikutano iliyofanyika kati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Gambia katika miaka ya hivi karibuni, hususan mazungumzo kati ya mwanadiplomasia mkuu wa Gambia Mamadou Tangara na Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Bagheri Kani mjini Tehran siku ya Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa taarifa ikitangaza kurejeshwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema:
Waziri wa Mambo ya Nje wa Gambia, Mamdou Tangara na Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Bagheri Kani walitangaza kurejeshwa uhusiano wa kidiplomasia jana Julai 29, 2024 ili kulinda maslahi ya mataifa yote mawili.
Vilevile serikali za nchi hizo mbili zimekubaliana kupanua mahusiano ya kirafiki kwa kuzingatia msingi wa kuheshimiana, usawa na maslahi ya pamoja.
Pande hizo mbili pia zimekubaliana kustawisha ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali; zikiwemo nyanja za kisiasa, kiuchumi, uwekezaji, biashara na uutamaduni, ambazo zinaweza kuhudumia maslahi ya mataifa yote mawili Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Gambia.