Iran na Afrika Kusini zatilia mkazo kuimarishwa uhusiano wa pande zote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i114648-iran_na_afrika_kusini_zatilia_mkazo_kuimarishwa_uhusiano_wa_pande_zote
Rais wa jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa uhusiano kati ya Iran na Afrika Kusini katika nyuga za pande mbili na pia ushirikiano wa kimataifa ukiwemo ule wa BRICS, na kusema: "Kwa kuzingatia uwezo uliopo, ninatumai kuwa uhusiano wa kiuchumi na ushirikiano wa kibiashara kati ya pande hizo mbili utaimarika zaidi na zaidi.
(last modified 2024-07-30T08:22:04+00:00 )
Jul 30, 2024 08:22 UTC
  • Pezeshkian na Ozzy Lamola
    Pezeshkian na Ozzy Lamola

Rais wa jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa uhusiano kati ya Iran na Afrika Kusini katika nyuga za pande mbili na pia ushirikiano wa kimataifa ukiwemo ule wa BRICS, na kusema: "Kwa kuzingatia uwezo uliopo, ninatumai kuwa uhusiano wa kiuchumi na ushirikiano wa kibiashara kati ya pande hizo mbili utaimarika zaidi na zaidi.

Dk Masoud Pezeshkian ameyasema hayo leo katika mazungumzo yake na Ronald Ozzy Lamola, Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, ambaye yuko mjini Tehran kwa ajili ya kushiriki katika sherehe za kuapishwa Rais wa Serikali ya Awamu ya 14 ya Iran.

Ameshukuru salamu za pongezi za Rais wa Afrika Kusini kwa mnasaba wa kupata imani ya taifa la Iran kwake, na pia salamu za rambirambi na masikitiko ya nchi hiyo baada ya kufa shahidi Dakta Ebrahim Raisi na kusema: Tunashukuru sana misimamo ya kisiasa na kirafiki ya Afrika Kusini, hasa hatua za serikali ya nchi hiyo ya kuwezesha na kuharakisha uanachama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kundi la BRICS.

Dk. Pezeshkian pia amepongeza misimamo mizuri ya Afrika Kusini katika kulitetea taifa madhulumu la Palestina na kusema: Utawala wa kibaguzi wa Israel haujaacha kufanya jinai zozote dhidi ya Wapalestina wanaodhulumiwa  wa Gaza; na hii ni pamoja na kwamba nchi zinazodai kutetea haki za binadamu zimenyamaza kimya mbele ya jinai hizo, bali zimechochea zaidi uhalifu huo kwa kutoa silaha na zana za kivita kwa Israel na kuhalalisha hatua za utawala huo wa Kizayuni.

Maelfu ya watoto wa Palestina wameuawa katika mashambulizi ya Israel

Kwa upande wake, Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, amewasilisha tena salamu za pongezi za Rais wa nchi yake kwa Dk Pezeshkian, pamoja na salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Dk Raisi, na kueleza nia ya nchi yake kuendeleza uhusiano wa pande mbili na wa kimataifa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikiwa ni pamoja na katika mfumo wa jumuiya ya BRICS.

Ronald Ozzy Lamola ameeleza kuwa, Afrika Kusini imekuwa ikikabiliwa na mashinikizo ya pande zote na hata vitisho kutokana na uungaji mkono wake kwa haki za watu wanaodhulumiwa wa Palestina hususan hatua yake ya kuwasilisha malalamiko dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika mahakama ya kimataifa. 

Amesema: Licha ya mashinikizo hayo yote, Afrika Kusini ina imani na misimamo yake kuhusiana na kadhia ya Palestina na itaendelea kufanya juhudi za pamoja na nchi kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika njia ya kutambua haki za watu wa Palestina na kufikiwa usitishaji vita wa kudumu huko Gaza na vilevile kuhakikisha misaada ya kibinadamu inapelekwa kwa Wapalestina wa eneo hilo.