"Mateka wa vita wa Iran ni nembo ya Muqawama dhidi ya adui"
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Mafungwa wa Vita ni nembo ya Muqawama na kusimama kidete taifa kubwa la Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya ubeberu na utwishaji wa maadui wa taifa hili.
Katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake ya mtandao wa kijamii wa X, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan'ani amesema, "(Leo) tarehe 26 Mordad (Agosti 16) tunaadhimisha kumbukumbu ya kurudi mateka mashujaa wa vita katika nchi yao."
Kan'ani amesisitiza kuwa, "Wafungwa wa vita ni alama za Muqawama, ustahimilivu na uimara wa taifa kubwa la Iran ya Kiislamu dhidi ya uchokozi, majivuno na kujitakia makuu maadui wa mipaka na ardhi hii iliyoweka historia."
Ameeleza bayana kuwa, "Tunaheshimu mapambano ya heshima na thabiti ya wafungwa hodari wa vita, na tunathamini juhudi zao za kuinua hadhi ya nchi na taifa azizi la Kiislamu la Iran katika medani za kimataifa."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, "Pia tunatoa pongezi kwa Mashahidi wote wa vita vya Kujihami Kutatifu (vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran mnamo 1980-1988) na kuwaenzi mateka wote wa vita hivyo walioachiwa huru."
Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo, kundi la kwanza la mateka wa Kiirani waliokuwa wakishikiliwa mateka katika magereza ya kutisha ya Saddam Hussein huko Iraq liliwasili katika ardhi ya Iran, ikiwa ni hatua muhimu ya kutekelezwa azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, baada ya Iraq kukubali mkataba wa mpaka wa Algeria.