Afrika Kusini na Somalia zalaani vikali shambulio la Israel nchini Iran
(last modified Mon, 28 Oct 2024 06:54:41 GMT )
Oct 28, 2024 06:54 UTC
  • Afrika Kusini na Somalia zalaani vikali shambulio la Israel nchini Iran

Afrika Kusini na Somalia zimelaani vikali shambulio la Jumamosi alfajiri la Israel dhidi ya Iran na kusema kuwa chokochoko hizo za utawala wa Kizayuni zinatishia usalama wa ukanda mzima wa Asia Magharibi.

Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imesema kuwa shambulio hilo la Israel ni ukiukaji usiokubalika wa haki ya kujitawala taifa la Iran na kuongeza kwamba, mbali na mauaji ya kimbari huko Ghaza, tayari uvamizi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan umesababisha mgogoro mkubwa na mbaya zaidi wa kibinadamu katika eneola Asia Magharibi na hivi sasa utawala huo umeanzisha chokochoko mpya dhidi ya Iran.

Vile vile taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imetoa mwito kwa Israel kukomesha mara moja jinai zake huko Ghaza, kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia wakazi wa eneo hilo na kuacha kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Israel inafanya jinai za kutisha mno huko Ghaza, Palestina

 

Kwa upande wake serikali ya Somalia nayo imetoa taarifa ya kulaani vikali mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Iran na kuitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dhati za kulinda usalama wa eneo la Asia Magharibi na watu wake.

Takriban Wapalestina 43,000 wameshauawa shahidi tangu Oktoba 7, 2023 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo. Wapalestina wengine zaidi ya 100,000 wameshajeruhiwa katika jinai hizo za kutisha za Israel. 

Mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni yamewalazimisha takriban wakazi wote wa Ukanda wa Ghaza kuwa wakimbizi na kuzuia kuwafikia misaada ya kibinadamu, na baya zaidi ni kuwafungia njia zote za kupata chakula, maji safi na dawa. Tayari Israel imefunguliwa mashitaka ya kujibu kesi ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki  (ICJ) kutokana na jinai zake za kutisha huko Ghaza.