Ghana kufungua tena Ubalozi wake Tehran mwezi huu wa Septemba
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ghana imesema kuwa Ubalozi wake hapa mjini Tehran, Iran, utaanza tena kazi zake Jumanne ya Septemba 16, baada ya kufungwa kwa muda.
Wizara hiyo imeeleza kuwa, uamuzi wa kufungua tena Ubalozi huo unatokana na kuimarika pakubwa hali ya usalama nchini Iran.
"Wizara ya Mambo ya Nje inapenda kuufahamisha umma kwamba, kutokana na kuimarika kwa hali ya usalama nchini Iran, uamuzi umefikiwa wa Ubalozi huo kuanza tena shughuli zake Jumanne, Septemba 16, 2025," imesema taarifa hiyo.
Wizara hiyo imesisitiza kwamba, itaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi katika ofisi hiyo ya kidiplomasia, pamoja na jamii ya Waghana hapa nchini Iran.
Ubalozi huo ulifungwa mnamo Juni 16, 2025, kama hatua ya tahadhari ya kuwalinda wafanyakazi wakati wa makabiliano makali kati ya Iran na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Uamuzi wa Ghana wa kurejesha shughuli za ubalozi nchini Iran unawiana na juhudi pana za mataifa ya Afrika kuimarisha uhusiano na mataifa yasiyo ya Magharibi.
Wakati Iran inapozidisha mawasiliano yake na eneo pana la kusini mwa dunia, kufunguliwa tena ubalozi huo kunaweza kuimarisha ushirikiano mpya wa kiuchumi na kimkakati.
Si vibaya kuashiria hapa kuwa, Ghana ni kituo cha kwanza kinachoongoza kupokea bidhaa za Iran zinazopelekwa barani Afrika.