IRGC: Israel isubiri jibu kali kwa kumuua kiongozi wa Hamas
Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesisitiza kuwa litalipiza kisasi mauaji yaliyotekelezwa na utawala wa Israel dhidi ya kiongozi wa ngazi ya juu wa Hamas, Ismail Haniyeh katika mji mkuu wa Iran, Tehran kwa jibu litakalokuwa kali na la nguvu zaidi kuliko wakati uliopita ambapo Jamhuri ya Kiislamu ililipiza kisasi dhidi ya uchokozi wa Tel Aviv.
Naibu Kamanda wa IRGC Brigedia Jenerali Ali Fadavi alitangaza Jumatatu kwamba utawala wa Kizayuni ulifanya uhalifu mkubwa kwa kumuua shahidi Haniyeh, na kwamba utaadhibiwa vikali zaidi kuliko wakati uliopita.
Jenerali Fadavi amesema adhabu hiyo itakuja “kwa wakati unaofaa na mahali muafaka.”
Ameongeza kuwa: "Ni sisi ndio tutaamua wakati na mahali pa kulipizia kisasi."
Haniyeh, mkuu wa zamani wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Wapalestina (HAMAS), aliuawa katika operesheni ya kigaidi jijini Tehran mwishoni mwa mwezi uliopita. Alikuwa katika mji mkuu wa Iran kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Masoud Pezeshkian wa Iran.
Mapema mwaka huu, IRGC ililenga Israel kwa ndege zisizo na rubani na makombora katika mfululizo wa mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyopewa jina la Operesheni ya Ahadi ya Kweli.
Operesheni hiyo ya kulipiza kisasi ilikuja baada ya utawala wa Israel kufanya mashambulizi ya anga ya kigaidi kwenye ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria Damascus, na kuwaua washauri wa ngazi za juu wa kijeshi pamoja na maafisa watano walioandamana nao.