Iran: Mbinu na muda wa jibu letu vitaishangaza mno Israel
Ofisi ya Uwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa imesema Jamhuri ya Kiislamu inapanga kwa makini muda na mbinu ya kulipiza kisasi cha mauaji ya kigaidi ya aliyekuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Wapalestina (HAMAS), Ismail Haniyah akiwa hapa Tehran.
Ofisi hiyo ya uwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa imesema katika taarifa ya Jumanne usiku kuwa, "Muda, masharti, na namna ya Iran kutoa majibu (dhidi ya Israel) yanapangwa kwa uangalifu ili kuhakikisha kwamba yanafanyika kwa kushtukiza na kwa muda usiotarajiwa; yumkini wakati macho yao yanaposhughulika kutazama angani na kwenye skrini zao za rada, tutawashtukiza kwa kuwashambulia kutoka ardhini, au labda hata kwa mchanganyiko wa wote mawili (mashambulizi ya ardhini na angani)."
Taarifa hiyo imeeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatoa "jibu kali" kwa kitendo cha ugaidi katika ardhi yake ili kuuadhibu na kuutia adabu utawala wa Kizayuni wa Israel.
Shahidi Haniyah aliuawa katika operesheni ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel hapa jijini Tehran mwishoni mwa mwezi uliopita. Alikuwa katika mji mkuu wa Iran kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais mpya wa Iran, Dakta Masoud Pezeshkian.
Ofisi ya Uwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa imeeleza katika taarifa hiyo kuwa, Iran itapanga kwa makini majibu yake "ili kuepusha athari yoyote mbaya ambayo inaweza kuathiri uwezekano wa kusitisha mapigano."
Taarifa ya ofisi hiyo ya kidiplomasia ya Iran katika Umoja wa Mataifa mjini New York inakuja wakati kukiwa na mjadala kuwa huenda Iran imechelewesha kwa makusudi majibu yake hadi matokeo ya mazungumzo ya kusitisha mapigano huko Gaza yatakapokuwa wazi.
Siku mbili za mazungumzo mjini Doha, kkwa upatanishi wa Qatar na Misri na kuzihusisha Marekani na Israel zilihitimishwa Ijumaa bila mafanikio, lakini mazungumzo zaidi yamepangwa kufanyika wiki ijayo mjini Cairo. Harakati ya Hamas imeyasusia mazungumzo hayo.