Iran yakosoa misimamo ya kindumakuwili ya Uingereza kuhusiana na vita vya Gaza
(last modified Mon, 26 Aug 2024 12:11:36 GMT )
Aug 26, 2024 12:11 UTC
  • Iran yakosoa misimamo ya kindumakuwili ya Uingereza kuhusiana na vita vya Gaza

Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini London umekosoa misimamo ya kindumakuwili ya serikali ya Uingereza kuhusiana na matukio ya eneo la Asia Magharibi na kusema, huku London ikionyesha kidhahiri kuwa inaunga mkono usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza, lakini imefumbia macho jinai za kutisha zinazofanywa na utawala wa Israel dhidi ya watu madhulumu wa Palestina.

Ubalozi huo umeandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kuwa, matamshi ya David Lemmy, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza kuhusu Asia Magharibi yanaweza kutafsiriwa kuwa ni uungaji mkono kamili kwa jinai za utawala wa Kizayuni na kuwa nchi nyingine zinapaswa kujizuia kukosoa jinai hizo.

Katika ujumbe huo, ubalozi wa Iran mjini London umesema madai ya Uingereza kuwa inaunga mkono usitishaji mapigano Gaza hayana msingi wowote kwa sababu haionyeshi kusikitishwa na maelfu ya wanawake na watoto wa Kipalestibna wanaoendelea kuuawa kinyama na utawala wa kibaguzi wa Israel kabla ya kufikiwa usitishaji mapigano.

Katika kipindi cha miezi 11 iliyopita, utawala wa Kizayuni umefanya mauaji makubwa ya kutisha huko Gaza ambapo umefunga vivuko vyote na kuzuia kuingizwa misaada ya kibinadamu katika ukanda huo huku ukibadilisha miundomsingi na majengo yake kuwa magofu. Vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni tarehe 7 Oktoba 2023 kwa malengo mawili ya kuangamiza harakati ya Hamas na kuwakomboa mateka wa Kizayuni bado havijafikia malengo hayo.

Miezi miwili iliyopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuunga mkono usitishaji vita huko Gaza, lakini Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni ambaye amepoteza uhalali wake katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na katika uga wa kimataifa anasisitiza juu ya kuendeleza vita hivyo vya maangamizi ya umati dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.

Tags