Iran: Dola ovu kabisa la Israel limekaribia mno kushindwa, si kushinda
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, kuendelea jinai za Israel na ndoto zake za kuchupa mipaka katika mazungumzo ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano, ni mambo ambayo yanaonesha kuwa utawala huo upo karibu zaidi kushindwa na si kushinda.
Nasser Kanani alisema hayo jana Jumatanu mbele ya waandishi wa habari hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa: "Utawala wa Israel ni uvimbe wa saratani na ni kiini kikuu cha mhimili wa uovu katika eneo hili."
Ameongeza kuwa, jinai za kutisha za Israel dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza na hivi karibuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan zimeongeza hasira na ghadhabu za kimataifa.
Vile vile ametilia mkazo dhamira ya Iran ya kisheria, kimaadili na ya kibinadamu ya kuiunga mkono Palestina na kuongeza kwamba, hatua ya utawala wa Kizayuni ya kuhusisha tukio lolote na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ushahidi wa kukata tamaa dola hilo na ni kujaribu kuficha ukweli.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran vilevile amelaani vikali mashambulizi ya utawala wa Kizayuni ya juzi Jumapili katika maeneo kadhaa ya kaskazini magharibi mwa Syria na amewataka wafuasi wa Israel kuacha kuupa silaha na kuuunga mkono utawala huo katili akisema kuwa, mashirika ya kimataifa yanatakiwa kulaani vikali jinai za utawala dhalimu wa Tel Aviv na kuchukua hatua madhhubuti za kukomesha jinai hizo za kutisha za Israel.