Ujumbe tofauti wa Kongamano la Umoja wa Kiislamu mjini Tehran
Kusadifiana jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza na kuenea jihai hizo hadi Lebanon kwa kulengwa kigaidi maelfu ya raia wa nchi hiyo kumeongeza maradufu haja ya kongamano la 38 mjini Tehran kutoa kipaumbele kwa mipango ya kuimarisha umoja wa kivitendo baina ya Waislamu na kuziwezesha nchi za Kiislamu kufikia nguvu moja ya kuzuia jinai za aina hiyo.
Kongamano la 38 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu linalofanyika mjini Tehran chini ya kaulimbiu ya "Ushirikiano wa Kiislamu na Kufikia Thamani za Pamoja kwa Kutilia Mkazo Suala la Palestina" lilianza jana asubuhi kwa hutuba ya Rais Masoud Pazeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo baadhi ya viongozi wa kijeshi na kisiasa pamoja na wanazuoni 78 wa kidini na kiutamaduni wa ulimwengu wa Kiislamu kutoka nchi 30 wanashiriki.
Katika ufunguzi wa kongamano hili, Rais Pezeshkian, alisema adui ameibua fitina na mifarakano baina ya Waislamu na kuongeza: "Mtume wa Uislamu Muhammad (saw) alianzisha umoja na udugu baina ya Waarabu na Waislamu, na sifa muhimu zaidi ya Mtume ni kuleta umoja na mshikamano baina ya Waislamu."
Kuwepo hitilafu na mifarakano baina ya Waislamu na nchi za Kiislamu kunaweza kutajwa kuwa tatizo na hatari kubwa zaidi inayotishia jamii za Kiislamu, na kuwa umoja na mshikamano baina ya Waislamu na nchi za Kiislamu ndilo suala muhimu zaidi linaloweza kutatua tatizo hilo.
Suala la ushirikiano na umoja baina ya nchi za Kiislamu lina historia ndefu kama inavyoonekana wazi katika nadharia za wanafikra wa Kislamu na fasihi ya kisiasa na kisheria ya Kiislamu ambapo ibara kama 'umma mmoja', 'daru salaam', 'umoja wa Kiislamu', 'muungano wa Kiislamu', 'umma wa Muhammad', 'kundi la Kiislamu', 'mrengo wa Kiislamu', 'ulimwengu wa Kiislamu', 'mshikamano wa kidini' na 'udugu wa Kiislamu' zimetumika kwa wingi.
Moja ya sababu za ulazima wa kuwepo umoja wa Kiislamu ni kunufaika na Uislamu kwa kiwango cha juu kabisa ambapo manufaa na maslahi ya jamii ya Kiislamu yanatoa udharura wa Waislamu kuungana kwenye mhimili mmoja. Ushindi na kuenea Uislamu katika miaka ya mwanzo ya dini hii ya mbinguni bila shaka kulitokana na mshikamano na umoja wa Waislamu. Umoja wa Umma wa Kiislamu ni hitajio la kijamii na kisiasa na ni jambo muhimu na la kistratijia na wala si suala la kimaonyesho tu.
Kwa kutegemea Aya za Qur'ani Tukufu na Hadith za viongozi wa kidini, Uislamu unasisitiza juu ya kusimamisha uadilifu na usawa katika jamii ya wanadamu na bila shaka lengo la kutumwa Mitume lilikuwa ni kusimamisha uadilifu katika jamii. Unasisitiza juu ya kuzingatiwa uadilifu katika nyanja zote za kijamii, kisiasa, kitamaduni na kiuchumi.
Moja ya siri za maendeleo na ushindi wa taifa lolote lile ni mshikamno na umoja wa watu wake. Moja ya njia muhimu za kufikia umoja ni kuwa na neno na msimamo mmoja kwenye mhimili wa Uislamu na kutekeleza maamrisho ya Uislamu. Kuna mambo mengi sana yanayoweza kuleta umoja kati ya Waislamu, ambapo kuna ushahidi na mifano mingi katika historia ambapo Mashia na Masunni wameshirikiana na kuonyesha umoja wao katika nyanja tofauti.
Bila shaka kama alivyosisitiza hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika moja hotuba zake, lau kama Waislamu na nchi za Kiislamu zingekuwa na umoja na mshikamano na kufikia mfumo wa usalama wa pamoja, tusingeshuhudia maafa na mauaji ya umati yanayofanywa leo na Wazayuni dhidi ya Waislamu huko Gaza na Lebanon.
Huko Gaza, karibu Waislamu milioni mbili na nusu wameuawa kwa umati, kujeruhiwa au kufukuzwa kwenye makazi yao huku Waislamu wenzao zaidi ya bilioni moja na nusu wakiwa wamekaa kimya na kutazama tu jinai hiyo ya kusikitisha ikitekelezwa na Wazayuni dhidi ya ndugu zao. Jinai kama hiyo imetekelezwa hivi karibuni huko Lebanon, ambapo matokeo ya ugaidi huo wa kimtandao wa Israel, umepelekea karibu Waislamu elfu nne kujeruhiwa katika siku moja na wengine kadhaa kuuawa shahidi. La kusikitisha ni kwamba mauaji hayo ya umati yangali yanaendelea na kuna hofu kuwa jinai inayofanywa na Wazayuni huko Gaza inapangwa kukaririwa nchini Lebanon. Kwa msingi huo kuna ulazima kwa Waislamu na nchi za Kiislamu kuchukua hatua za kivitendo za kuimarisha umoja na mshikamano wao wa ndani kwa njia yoyote ile inayowezekana ili kukabilina vilivyo na maadui wao.
Kwa mtazamo huu, inatazamiwa kwamba mara hii Kongamano la 38 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu mjini Tehran litakuwa tofauti na makongamano mengine yaliyopita. Makongamano haya yamekuwa yakifanyika tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa lengo la kuimarisha umoja baina ya Waislamu, na ingawa yamefanikiwa katika kuyaleta pamoja madhehebu ya Kiislamu, lakini kwa kuzingatia matukio ya sasa katika ulimwengu wa Kiislamu kuna haja ya umoja huo kuimarishwa na kuendelezwa zaidi kutoka kwenye duru za wasomi na wanafikra wa Kiislamu na kuenezwa katika jamii na serikali za Kiislamu. Suala hilo bila shaka litaharakisha mwenendo wa maendeleo na umoja wa nchi na jamii za Kiislamu na wakati huo huo kuunda nguvu kubwa ya Kiislamu kwa ajili ya kuzuia hujuma na njama za wapinzani na maadui wa Uislamu.