Hatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran asisitiza umuhimu wa umoja wa Waislamu
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran ametilia mkazo umuhimu wa kuimarishwa umoja na mshimakamano baina ya Waislamu kote duniani na kujiepusha na jambo lolote linaloibua hitilafu na mifarakano baina ya wafuasi wa dini hiyo.
Hujjatul Islam Walmuslimin Abu Tarabifard amesema: Waislamu wote wana mwelekeo mmoja na ni lazima waheshimiane na kuwafuata wanazuoni mashuhuri wa Ulimwengu wa Kiislamu kama Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei na hayati Imam Khomeini mbao wanalingania umoja na mshikamano baina ya makundi yote ya Waislamu na kutahadharisha juu ya mifarakano na hitilafu.
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran, ameashiria kauli ya Imam Ali bin Abi Twalib (AS) ambaye amesema, hitilafu na mifarakayo inayotokea baina ya watu si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, bali chanzo chake ni masuala ya kidunia na kusema: Athari za udhaifu na mporomoko wa kiutamaduni, kisiasa, kiuchumi na kijeshi zilionekana hatua kwa hatua katika Ulimwengu wa Kiislamu sambamba na kuwasili kwa ukoloni wa Ulaya katika ardhi za Waislamu.
Hujjatul Islam Abu Tarabifard amesema: Katika kipindi chote cha karne ya 19 na 20 madola ya kikoloni ya Ulaya yalikabiliana na kugombana wao kwa wao kwa ajili ya kupora mali ya Ulimwengu wa Kiislamu, lakini yalikubaliana kubakisha mataifa ya Waislamu katika hali ya dhaifu na unyonge na kuyagawa mataifa hayo. Amesisitiza kuwa Uingereza lilikuwa na nafasi kuwa zaidi katika njama hiyo.
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amesema, madola hayo ya kikoloni hususan Marekani yanafanya jitihada kubwa za kuzuia juhudi zote za kuimarishwa uhusiano wa kidini, kisiasa na kiuchumi baina ya Waislamu na kurejeshwa nguvu ya Umma wa Kiislamu. Amesisitiza kuwa yanatumia nguvu zao zote kutimiza malengo yao yakisaidiwa na wasomi waliouza nafsi zao kwa madola ya kikoloni.
Katika sehemu moja ya hotuba zake za Swala ya Ijumaa ya leo, Hujjatul Islam Walmuslimin Abu Tarabifard amesema, hii leo utawala wa Kizayuni wa Israel umepoteza uwezo wake wa kujilinda na unajiona kuwa uko katika hatari na tishio kubwa. Amesema: Utawala huo unakabiliwa na mporomoko mkubwa wa kiusalama na unazongwa na migogoro mikubwa ya kiuchumi na kisiasa.