Rais wa Iran asisitizia umuhimu wa umoja wa Waislamu
(last modified Fri, 11 Oct 2024 11:18:28 GMT )
Oct 11, 2024 11:18 UTC
  • Rais wa Iran asisitizia umuhimu wa umoja wa Waislamu

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amesisitiza haja ya umma wa Kiislamu kuwa na umoja na mshikamano na kubainisha kwamba, migawanyiko kati ya Waislamu itawanufaisha maadui pekee.

Rais wa Iran amesema hayo leo huko Ashgabat, Turkmenistan na kuongeza kuwa: Wito wa umoja hauhusu tu umma wa Kiislamu; lakini imekuwa hitaji la dharura kwa jumuiya ya kimataifa kuunda umoja huo.

Dakta Pezeshkian amesema hayo wakati wa hotuba katika sherehe ya kuadhimisha miaka 300 tangu kuaga dunia kwa mshairi maarufu wa Kiturukmenistan "Makhtumgoli Faraghi" huko Ashgabat. Amebainisha kuwa, sehemu muhimu za historia, fasihi na utamaduni wa watu wa Iran zimeunganishwa sana na ustaarabu wa Asia ya Kati.

Katika hatua nyingine, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin wamekutana na kufanya mazungumzo kuhusiano wa pande mbili huko nchini Turkmenistan leo Ijumaa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ria Novosti, Rais wa Russia amemwambia mwenzake wa Iran kwamba, nchi hizo mbili zina maoni kuhusu matukio ya kimataifa.

Hii ni mara ya kwanza kwa Marais wa Iran na Russia kukutana

Aidha kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, Pezeshkian, kwa upande wake, amesema kuwa, "Uhusiano wetu na Russia ni wa dhati na wa kimkakati."

"Katika nyuga za uchumi na utamaduni, uhusiano wetu unazidi kuimarika na unaboreka zaidi kadri muda unavyosonga mbele. Mwenendo unaokua wa ushirikiano kati ya Iran na Russia unapaswa kuharakishwa kwa mujibu wa matakwa ya viongozi wakuu wa nchi hizo mbili na ulazima wa kuimarishwa uhusiano huo," amesisitiza Rais wa Iran.