Iran yasisitiza kuwa bila shaka itajibu uchokozi wa Israel
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei amesema bila ya shaka utawala wa Kizayuni wa Israel utapokea jibu kali kutokana na uchokozi wake wa hivi karibuni dhidi Iran.
Baghaei amewaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu kwamba: "Tutatumia rasilimali zetu zote za kimaada na kimaanawi kujibu hujuma za utawala wa Kizayuni (Israel) ”
Alipoulizwa iwapo kutakuwa na mabadiliko ya jibu la Iran kwa uchokozi wa Israel endapo kutakuwa na usitishaji vita huko Gaza, Baghaei amesema mauaji ya kimbari ya Israel huko Palestina na uchokozi nchini Lebanon ndio masuala makuu, na "tunaunga mkono mipango ya kukomesha uhalifu."
Akihutubia kikao cha baraza la mawaziri siku ya Jumapili, Rais Pezeshkian alisema mapatano huko Gaza na kukomesha mauaji ya Israel kwa raia "vinaweza kuathiri" majibu ya kijeshi ya Iran kwa Israel.
Hata hivyo amesisitiza kuwa Iran haitaacha "bila majibu" kitendo chochote cha uchokozi dhidi ya mamlaka na usalama wake.
Baghaei pia amekosoa uwepo wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi na kusema uwepo huo unavuruga utulivu huku akizitaka nchi za eneoo kutatua matatizo ya kupitia mashauriano.
Baghaei pia amesema uchaguzi wa Marekani ni suala la ndani lakini utendaji wa marais waliochaguliwa ni muhimu kwa Iran.
Amebainisha kuwa kulingana na historia, hakuna tofauti kubwa kati ya viongozi wa Marekani kuhusu sera na mtazamo wao kuhusu Iran.