Iran yaonya kuhusu kuenea kwa vita vya Israel nje ya Asia Magharibi
(last modified Sun, 10 Nov 2024 03:43:13 GMT )
Nov 10, 2024 03:43 UTC
  • Iran yaonya kuhusu kuenea kwa vita vya Israel nje ya Asia Magharibi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi ameonya kwamba matokeo mabaya ya uvamizi wa kikatili wa Israel kwenye Ukanda wa Gaza na kusini mwa Lebanon hayataishia Asia Magharibi na yanaweza kusambaa zaidi ya eneo hilo la kimkakati

Araghchi amesema hayo katika mkutano wa kilele wa kimataifa uliopewa jina la Fikra za Nasrullah', ambao ulifanyika katika kumbukumbu ya Arubaini ya shahidi kiongozi wa Hizbullah Sayyed Hassan Nasrullah. 

Araghchi amesema: “Utawala wa Israel ambao ni utawala ghasibu, wa ubaguzi wa rangi na muuaji wa watoto, umekataa mipango na mapendekezo yote ya usitishaji vita huko Gaza na Lebanon,  na sasa unaendelea na jinai zake huko Palestina na Lebanon, na cha kusikitisha ni kwamba jumuiya ya kimataifa imeshindwa kukomesha mauaji hayo ya kimbari yanayotekelezwa na Wazayuni."

Ameongeza kuwa: “Ulimwengu unapaswa kujua kwamba iwapo vita hivyo vitapanuka, madhara yake hayataishia katika eneo la Asia Magharibi pekee; ukosefu wa usalama na ukosefu wa utulivu ni jambo ambalo linaweza kuenea katika maeneo mengine, hata yaliyo mbali kabisa."

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran amesema kutekelezwa usitishaji vita wa haki huko Gaza na Lebanon kunapaswa kuwa "kipaumbele" cha jumuiya ya kimataifa, akisisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu imetekeleza kila juhudi kuhusiana na usitishaji vita.

Kwingineko katika hotuba yake, Araghchi amemsifu Shahidi Nasrullah na kumtaja kuwa ni nembo ya muqawama au mapambano ya Kiislamu, ujasiri na kusimama dhidi ya dhulma na uchokozi sio tu kwa Lebanon bali pia kwa ulimwengu wa Kiislamu na mataifa yote yanayopigania uhuru.