Indhari ya Iran kuhusu mchezo wa kisiasa wa Troika ya Ulaya
(last modified Sun, 17 Nov 2024 02:26:06 GMT )
Nov 17, 2024 02:26 UTC
  • Indhari ya Iran kuhusu mchezo wa kisiasa wa Troika ya Ulaya

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo na Rafael Grossi Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa KImataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) hapa Tehran kuwa: "Kile ambacho Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakitaka katika teknolojia ya nyuklia kinakwenda sambamba kikamilifu na mifumo na vibali vya kisheria vya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: "Kama tulivyothibitisha nia yetu njema huko nyuma na mara kwa mara, tunatangaza kuwa tuko tayari kushirikiana na kwenda sambamba na taasisi hiyo ya kimataifa kwa lengo la kuondoa shaka zinazotokana na madai kuhusu shughuli za nyuklia za Iran zinazofanyika kwa malengo ya amani; ingawa leo hii dunia pia inaamini kuwa Iran ya Kiislamu inataka dunia yenye amani na usalama."

Katika mazungumzo ya siku ya Jumatano na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa IAEA, Pezeshkian aliashiria pia makubaliano ya JCPOA na uvunjaji wa ahadi na kutowajibika Marekani na nchi za Ulaya katika makubaliano hayo na kusema: 'Ripoti kadhaa zilizothibitishwa na IAEA zinaonyesha kuwa Iran imetekeleza majukumu yake yote kwa mujibu wa makubaliano hayo hata hivyo ni Marekani ambayo ilijitoa kwa upande mmoja katika makubaliano hayo na kukwamisha kuendelea kwa mchakato huo.' 

Katika mazungumzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia pia amepongeza mtamzamo wa kupenda amani na maelewano wa serikali ya Rais Pezeshkian na  akapongeza pia ushirikiano wa dhati kati ya maafisa wa Shirika la Nishati ya Nyuklia, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na IAEA. Rafael Grossi alitoa tathmini jumla ya uhusiano na maelewano mazuri kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na IAEA na kusema: 'Tunaamini kwa dhati duru ya uongozi wako itafungua ukurasa mpya wa uhusiano mwema na chanya kati ya Iran na wakala wa IAEA.'

Rafael Grossi pia alituma ujumbe katika mtandao wa kijamii wa X kuhusu mazungumzo kati yake na Rais Masoud Pezeshkian wa Iran ambapo aliandika: ''Mazungumzo niliyofanya na Rais Masoud Pezeshkian wa Iran ni sehemu muhimu ya safari yangu, na ni fursa kwa ajili ya mazungumzo na serikali mpya ya Iran ili kusikia mitazamo yake, na kuibainisha mbinu na jitihada zangu mkabala wa moja ya kadhia zenye changamoto kubwa kimataifa." 

Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA
 

Ukweli wa mambo ni kuwa baadhi ya madai kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani yanarejea nyuma kwa kesi zilizokwishapatiwa ufumbuzi katika mazungumzo yaliyopelekea kufikiwa makubaliano ya JCPOA, hata hivyo hatua ya Marekani kujitoa kwa upande mmoja katika makubaliano hayo na utawala wa Kizayuni kuushinikiza wakala wa IAEA, kwa mara nyingine tena kuliibuliwa masuala hayo ya huko nyuma yakitajwa kuwa kadhia zenye kuzusha hitilafu ili kuishinikiza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Licha ya kuwepo masuala ya kisiasa kuhusu nafasi ya usimamizi na kiufundi ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifanya kila ilichoweza kushirikiana na wakala huo ili kuhitimisha madai yaliyokuwa yamepatiwa ufumbuzi hata hivyo pande za Magharibi ziliendelea kuvuruga na kukwamisha mchakato wa ushirikiano kati ya Iran na IAEA kama wenzo wa mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Katika hali ambayo Rafael Grossi amefanya safari Tehran kwa shabaha ya kushauriana na kuzungumza na viongozi wa Iran kwa ajili ya kuendeleza ushirikiano na kutatua kadhia zenye kuibua hitilafu na mivutano; lakini baadhi ya vyombo vya habari vimewanukuu wanadiplomasia na kuripoti kuwa serikali za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zinafanya kila ziwezalo ili kuwasilisha azimio dhidi ya Iran katika kikao cha msimu cha wiki ijayo cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia. 

Katika mazungumzo na Rafael Grossi mjini Tehran, viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametangaza kuwa wako tayari kushirikiana kikamilifu na wakala huo katika fremu ya makubaliano ya NPT na kukabiliana na mashinikizo yoyote ya kisiasa. 

Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alimweleza Rafael Grossi kuhusiana na suala hilo kwamba: "Hakuna njia yoyote ya mantiki iliyopo isipokuwa njia ya mazungumzo kwa ajili ya kutatua matatizo yaliyopo. Njia ya makabiliano ilishatumika huko nyuma na wanaweza kuijaribu tena pia katika siku za usoni."

Naye Muhammad Eslami Mkuu wa Shirika la Nishati ya Nyuklia la Iran alisema katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Rafael Grossi kuwa: "Azimio lolote litakalowasilishwa kuhusu masuala ya nyuklia ya Iran litakabiliwa na jibu la haraka la Tehran. Wana uzoefu wa mara nyingi kwamba Iran haitaathiriwa na mashinikizo na itasonga mbele na miradi yake kwa mujibu wa maslahi yake ya taifa". 

Rafael Grossi (kushoto) na Muhammad Eslami katika mkutano na waandishi wa habari