Pezeshkian: Upanuzi wa uhusiano na Qatar ni muhimu kwa Iran
Rais Masoud Pezeshkian amesema Iran inaupa umuhimu mkubwa upanuzi wa uhusiano na jirani na rafiki yake, Qatar.
Rais Pezeshkian aliyasema hayo jana Jumatano alipokutana na Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani katika mji mkuu Tehran.
Pezeshkian amesema Tehran itaharakisha utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na Doha katika ziara yake ya hivi majuzi katika nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi.
Rais wa Iran ameelezea matumaini yake kuwa upande wa Qatar pia utatekeleza makubaliano hayo kwa azma kubwa zaidi.
Pezeshkian pia ameangazia maono yake ya umoja katika ulimwengu wa Kiislamu.
Amesema: "Nia yetu ya dhati ni kuwa na uhusiano wa dhati na ndugu zetu Waislamu na kuuonyesha ulimwengu kwamba nchi za Kiislamu zinaweza kuishi pamoja kwa amani na maelewano, zikiheshimiana, huku zikibadilishana uzoefu na kushirikiana bega kwa bega."
Wakati wa ziara rasmi ya Pezeshkian nchini Qatar mapema Oktoba, maafisa wa Iran na Qatar walitia saini mikataba sita ya ushirikiano.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar kwa upande wake ameeleza nia ya nchi yake katika kupanua uhusiano na Iran na kusema kuwa Doha inatumai kuwa Amir wa Qatar atazuru Iran mapema mwaka ujao.
Amesema viongozi wa Qatar akiwemo Emir na wakuu wengine wa serikali ya Qatar wanasisitiza haja ya kuharakisha utekelezaji wa makubaliano kati ya nchi hizi mbili.