Baqaei: Iran ilikuwa Syria kukabiliana na ugaidi na kwa mwaliko wa serikali
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran anasema Iran ilituma washauri wa kijeshi nchini Syria kwa ajili ya kusaidia nchi hiyo kupambana na ugaidi na kwamba itafunguliwa tena ubalozi wake nchini humo mara tu "mazingira yanayohitajika" yatakapoandaliwa.
Esmaeil Baqaei amesema kuwa kutumwa kwa washauri wa kijeshi wa Iran nchini Syria lilikuwa jambo la msingi na liliegemezwa katika kanuni na sheria, na kuondoka kwao nchini Syria pia ni hatua ya kuwajibika.
"Hatukwenda kuikalia kwa mabavu Syria wala kufufua utawala wa zamani. Kilichokuwa muhimu nchini Syria ni kusaidia kuhakikisha usalama na amani ya umma dhidi ya makundi ya kigaidi", amesema Baqaei.
Amesema Iran ilituma washauri wa kijeshi nchini Syria kwa mwaliko wa serikali ya zamani ya Syria na haikwenda kusaidia mtu au kikundi fulani. "Ilikuwa muhimu kwetu kusaidia juhudi za kulinda mamlaka ya kujitawala ya Syria na tunaamini kwamba kuwepo usalama katika nchi za kikanda kunahakikisha usalama katika eneo zima la Asia Magharibi," amesema Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran.
Amelaani vitendo vya hivi karibuni vya Israel dhidi ya Syria, na kusema kwamba mamlaka ya ardhi ya taifa hilo la Kiarabu imehujumiwa na sehemu ya ardhi yake imekaliwa kwa mabavu kinyume na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.