Rais Pezeshkian aelekea Cairo kwa ajili ya mkutano wa D8
-
Rais Masoud Pezeshkian
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian ameelekea Cairo, mji mkuu wa Misri, kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa 11 wa nchi nane zinazoendelea za Kiislamu zinazojulikana kwa jina la D8.
Katika safari hii, mbali na kushiriki katika mkutano wa kilele wa D8, Rais Pezeshkian pia atakutana na kufanya mazungumzo ya pande mbili na baadhi ya viongozi na maofisa wanaoshiriki katika mkutano huo na kujadili masuala ya pande mbili, kikanda na kimataifa.
Mkutano wa 11 wa kilele wa nchi nane zinazoendelea za Kiislamu, kwa kifupi D8, umepangwa kufanyika kesho Alkhamisi mjini Cairo, ili kujadili njia za kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kisiasa katika Ulimwengu wa Kiislamu.
Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Kiuchumi ya D8 ambayo inajumuisha pamoja nchi nane za Kiislamu zinazoendelea ambazo ni Iran, Uturuki, Misri, Pakistan, Indonesia, Nigeria, Malaysia na Bangladesh, umefanyikka leo Jumatano, Disemba 18, yaani siku moja kabla ya mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa D8 utakaofanyika kesho Alkhamisi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araqchi anawakilishi Jamhuri ya Kiislamu katika mkutano huo.
Miongoni mwa mada kuu za mkutano wa kesho wa viongozi wa D8 ni "Kuwekeza kwa ajili ya Vijana na Kusaidia Biashara Ndogo Ndogo na za Kati pamoja na Kuunda Uchumi wa Baadaye."