Mahusiano ya Biashara ya Iran na Pakistan yaongezeka
Takwimu zinaonyesha kuwa, uhusiano wa kibiashara wa Iran na Pakistan umeongezeka na unazidi kukua siku baada ya siku.
Mwaka jana (2023), uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na Pakistan uliongezeka, kwa asilimia 8 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake, na kufikia kiasi cha dola bilioni 2.7.
Mwenendo huu wa kutia moyo unaungwa mkono na hatua kadhaa za kimkakati kutoka kwa nchi zote mbili. Hatua hizo ni pamoja na ziara za mara kwa mara za viongozi wa ngazi ya juu kwa ajili ya kufikia lengo la mabadilishano ya biashara la dola bilioni 10 kwa mwaka.
Miongoni mwa hatua muhimu zilizochukuuliwa na mataifa haya mawili, ni kuboresha masoko ya mpakani na kuandaa maonyesho mengi ya biashara ili kuonyesha bidhaa zao.
Inaelezwa kuwa, kufikia mwishoni mwezi Machi 2025, juhudi hizi zinaweza kuzaa matunda makubwa na hivyo kuboresha zaidi kiwango cha biashara kati ya mataifa haya mawili jirani ya Kiislamu.
Pakistan, yenye wakazi zaidi ya milioni 240, iko kati ya masoko makubwa zaidi katika eneo. Mauzo yake ya msingi kwa Iran yanajumuisha bidhaa za kilimo, nguo, na malighafi ya viwanda. Kwa upande mwingine, mchango mkubwa wa Iran katika uhusiano huu wa kibiashara ni pamoja na bidhaa za petrokemikali na bidhaa za kilimo.