Blinken: Marekani haina uwezo wa kupindua serikali ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i120446-blinken_marekani_haina_uwezo_wa_kupindua_serikali_ya_iran
Anthony Blinken Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani sambamba na kukiri kuweko njama za Marekani za kuihujumu Iran, ameeleza kwa kina sababu zinazofanya juhudi hizo kutozaa matunda.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 22, 2024 00:11 UTC
  • Blinken: Marekani haina uwezo wa kupindua serikali ya Iran

Anthony Blinken Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani sambamba na kukiri kuweko njama za Marekani za kuihujumu Iran, ameeleza kwa kina sababu zinazofanya juhudi hizo kutozaa matunda.

Blinken amesema hayo katika mahojiano na Chuo cha Baraza la Mahusiano ya Kigeni mjini New York na kueleza kwamba, njama za Marekani za kuiangusha serikali ya Iran zimefeli.

Katika kujibu swali la mwendesha kipindi kuhusu iwapo Marekani inapaswa kuweka sera ya kubadilisha utawala nchini Iran kwenye ajenda zake, Blinken alikumbusha kwamba "majaribio ya Marekani ya mapinduzi" katika kipindi cha miaka 20 iliyopita hayajakuwa na matokeo yenye mafanikio.

Katika kujibu madai ya mtangazaji  kwamba serikali ya Iran "haipendwi sana" ndani ya nchi, alisema: "Kwa mtazamo wangu, kwanza kabisa, matukio ya ndani ya Iran ni tata na kutokana na sababu kadhaa, sisi sio lazima kuwa chanzo bora cha kuwa na maoni wazi juu ya hili kwa sababu hatuna uhusiano wa kidiplomasia na hakuna maingiliano yanayoendelea kati yetu."

Ikumbukwe kuwa, kwa miongo minne na ushei sasa ambapo Marekani imekuwa ikifanya kampeni za chuki na hata njama za kutaka kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaotawala hapa nchini.

Hata hivyo njama zote za Marekani na washirika wake zimegonga mwamba ambapo hata vikwazo na mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Iran navyo havijafua dafu.