Qalibaf: Iran imesimama imara kuwatetea Waislamu duniani
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema: Iran siku zote inasisima imara na imeonyesha kuwa ni nchi pekee inayowatetea Waislamu wote bila ya kujali madhehebu zao na imetoa maelfu ya mashahidi katika njia hii.
Mohammad Bagher Qalibaf, ambaye yuko katika ziara ya siku mbili nchini Ethiopia kufuatia mwaliko wa Tagse Chafo, Spika wa Bunge la nchi hiyo na kwa minajili ya kustawisha uhusiano kati ya mabunge ya nchi mbili, ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Sheikh Ibrahim Tufa, Mkuu wa Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu la Ethiopia au 'Majlis".
Qalibaf amesisitiza umuhimu wa umoja kati ya madhehebu za Kiislamu na kusema: Kuna madhehebu mbalimbali nchini Iran na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, yaani Bunge, ina wawakilishi wa Kishia na Kisuni na pia wafuasi wa dini zingine kama Wakristo, Wayahudi na Wazoroastria.
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameashiria uwepo wa Waislamu wa Kisuni serikalini na kuongeza kuwa: Hivi sasa, wawakilishi 26 wa Kisuni wapo katika Bunge la Iran, na Wasuni pia wanashika nyadhifa mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais, Magavana na Manaibu Mawaziri.
Katika mazungumzo hayo, Sheikh Ibrahim Tufa pia ameashiria hali ya Waislamu nchini Ethiopia na kusema: Zamani Waislamu katika nchi hiyo walikabiliwa na matatizo mengi, lakini kwa kuzingatia mabadiliko ya hali ya kisiasa na kuingia madarakani Waziri Mkuu wa sasa, Waislamu wanatangaza dini yao kwa uhuru kabisa.