Sababu za kukua uchumi wa Iran licha ya kukabiliwa na vikwazo
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imestawi pakubwa kiuchumi licha ya vikwazo na sera za Marekani na nchi za Magharibi dhidi yake.
Abdolnaser Hemmati Waziri wa Uchumi na Fedha wa Iran amebainisha kuhusu ukuaji wa kiuchumi na kibiashara wa Iran katika miezi 10 iliyopita. Takwimu mpya za ukuaji wa uchumi wa Iran zimechapishwa katika hali ambayo Marekani na nchi za Magharibi zimeshadidisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran katika miezi ya hivi karibuni kwa visingizio vya uwongo.
Abdelnaser Hemmati Waziri wa Uchumi na Fedha wa Iran ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii kwamba: Kulingana na takwimu za karibuni za forodha za biashara isiyo ya mafuta katika miezi 10 iliyopita tangu mwanzoni mwa mwaka 1403 hijria shamsiya; uuzaji nje bidhaa zisizo za mafuta ulifikia dola bilioni 47.8, kiwango ambacho kimeongezeka kwa asilimia 18 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita wa 1402.
Waziri wa Uchumi na Fedha wa Iran ameongeza kuwa: Uagizaji bidhaa kutoka nje uliongezeka kwa asilimia 3 yaani dola bilioni 56 katika kipindi sawa na hicho (ikiwa ni pamoja na dhahabu za dola bilioni 3.6). Waziri wa Uchumi na Fedha wa Iran pia ameandika kuwa: Ziada ya mlingano wa mauzo ya bidhaa za mafuta na zisizo za mafuta ilifikia zaidi ya dola bilioni 28 ikijumishwa na zaidi ya dola bilioni 30 za uuzaji mafuta nje ya nchi katika kipindi hicho.
Hemmati pia amesisitiza kuwa: Masuala ya kigeni yanaweza kusababisha matatizo kwa sekta ya uchumi, lakini heshima na hadhi ya taifa haiwezi kupuuzwa mbele ya mashinikizo ya maadui. Tuna mpango wa kushughulikia matatizo yote yanayoweza kutokea.
Katika ripoti yake mpya, Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) umetabiri kuwa Pato la Taifa la Iran litakuwa kwa asilimia 1.3 mwaka huu wa 2025.
Baada ya vikwazo vya miaka kadhaa vya Marekani na Magharibi dhidi yake, Iran inaendelea kufanya juhudi za kuboresha uhusiano wake na nchi nyingine kwa upande wa kiuchumi; na wakati huo huo kujenga upya uwezo wake wa kiuchumi kupitia kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na yasiyo rasmi na maafisa husika wa nchi mbalimbali ili kuandaa mazingira chanya zaidi kwa jaili ya uwekezaji kutoka nje.
Wakati huo huo Iran inaweza kutoa kipaumbele kwa suala la kuwavutia wawekezaji ili kuwekeza hapa nchini kwa kuzingatia uwezo wake mkubwa katika nyanja mbalimbali kama vile mafuta na gesi, migodi, sekta ya chakula na teknolojia.
Mipango na malengo ya muda mrefu ya kiuchumi kwa miaka ijayo yamekuwa sehemu ya mbinu muhimu zaidi za serikali tofauti za Iran katika miaka iliyopita kwa ajili ya uzalishaji na ustawi wa kiuchumi.
Nchini Iran, sehemu muhimu ya uzalishaji hufanyika viwandani na katika vitengo vyake; ambapo aghalabu ya vitengo hivi ni sehemu ya kundi kubwa la viwanda vya msingi kama vile vinavyozalisha saruji, chuma, shaba, alumini na sekta nyingine za viwanda.
Uuzaji wa mafuta na gesi nje ya nchi pia unadhamini sehemu muhimu ya pato la fedha za kigeni la Iran ambalo limeongezeka kwa kiasi kikubwa,; na licha ya mashinikizo ya Marekani na makampuni makubwa ya mafuta yenye mfungamano na nchi hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kulinda soko lake katika nchi mbalimbali na kustawisha sekta yake ya petrokemikali.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezitilia maanani na kutoa zingatio maalumu kwa nchi jirani katika kalibu ya mipango na malengo yake ya kupanua ushirikiano wa kiuchumi; ambapo imetenga sehemu kubwa ya uuzaji nje na uagizaji wa bidhaa kwa ajili ya nchi hizo. Iran pia katika miaka ya karibuni imejikita katika kuwekeza katika nchi za bara la Afrika na Asia Mashariki na kustafidi na uwezo wa kiuchumi wa nchi hizo.
Mtazamo huu wa kiuchumi wa Iran umekaribishwa pakubwa na nchi za kanda hii, na kigezo cha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na nchi jirani umepongezwa na wachumi, taasisi na mashirika makubwa ya kiuchumi.