Mafanikio mapya ya kiulinzi ya Iran yana jumbe gani?
Ikiwa ni katika muendelezo wa kuzindua mafanikio ya kiulinzi ya Iran, Jumapili ya jana tarehe Pili Februari, Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kilizindua kituo kipya cha chini ya ardhi.
Uzinduzi huo ambao ni mlolongo wa sehemu ya kumbukumbu ya Alfajiri Kumi kuelekea kilele cha maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran umefanyika katika maeneo ya mwambao wa kusini mwa Iran ambapo kituo hicho kiipya cha chini ya ardhi kinahifadhi makombora yaliyo tayari kuteketeza manowari za mashambulizi za adui katika eneo la kimkakati la majini.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, (SEPAH) Meja Jenerali Hossein Salami na Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha jeshi hilo Admirali Ali Reza Tangsiri walizindua kituo hicho cha makombora ya kushambulia manowari sambamba na kukagua hali ya utayarifu wa kivita ya Kikosi cha Wanamaji cha SEPAH.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Sepah News, makombora hayo ya kruzi aina ya Qadr 380 yenye uwezo wa kukabiliana na vita vya kielektroniki vya manowari za mashambulizi yanahifadhiwa katika mji mpya wa makombora wa chini ya ardhi wa IRGC, au Sepah.
Makombora hayo ambayo yamefanyiwa maboresho makubwa ya mifumo yao ya silaha na hatua za kielektroniki za kukabiliana na mashambulizi ya kivita, yanaweza kutumwa kushambulia ndani ya muda mfupi kabisa.
Makombora ya kruzi ya Qadr 380 yanafika umbali wa zaidi ya kilomita elfu moja katika kushambulia na yana uwezo wa kuongozwa hadi yanapopiga shabaha iliyokusudiwa.
Makombora hayo yameundwa kwa namna ambayo hayawezi kubabaishwa na kupoteza shabaha. Sifa nyingine ya makombora ya Qadr 380 ni kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa kuongozwa na mtu mmoja na kutekeleza operesheni za mashambulizi katika muda wa chini ya dakika tano.
Admeri Alireza Tangsiri, kamanda wa Jeshi la Wanamaji la IRGC alisema: Mifumo hii ya makombora na miji inaweza kuwa na silaha mamia ya kilomita kutoka kwenye kina cha nchi, kurusha na kulenga shabaha zao ndani kabisa ya bahari.
Katika siku na miezi ya hivi karibuni, miji ya kijeshi ya chini ya ardhi imezinduliwa katika maeneo tofauti ya kijiografia ya Iran. Kuzinduliwa kwa miji hiyo ya chini kwa chini na vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kunatuma jumbe kadhaa muhimu.
Moja ya jumbe muhimu ni kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatilia mkazo sana suala la kuimarisha uwezo wake wa kijeshi katika nyuga mbalimbali zikiwemo za baharini. Mtazamo huu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatokana na umuhimu inaouweka katika kukuza uwezo wa kujikinga kijeshi.
Ujumbe mwingine muhimu ni kwamba, vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinasasisha na kuujadidisha uwezo wao wa kijeshi kwa mujibu wa vitisho.
Ujumbe mwingine muhimu wa kuzunduliwa miji hiyo ya chini kwa chini ni kwamba, adui asifanye makosa ya tathmini katika kukadiria uwezo wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kabla ya hapo, Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) alisema: "Miji hii ya makombora ni sehemu ya nguvu zetu. "Kuzinduliwa kwa miji ya makombora ni kufanya hesabu za maadui kuwa sahihi zaidi ili wasifanye makosa, kwa sababu makosa yao yanaweza kuwatumbukiza wao na wengine kwenye matatizo makubwa."
Moja ya ujumbe muhimu zaidi wa kuzinduliwa miji ya chini ya ardhi ni kulinda kanuni na misingi ya kiulinzi na kiusalama.
Kipengele muhimu zaidi cha vituo na miji ya kijeshi ya chini ya ardhi, ikiwa ni pamoja na IRGC na jeshi, ni maeneo yake kuwa ni ya siri na yasiyotambulika. Kipengee hiki kinapunguza vitisho vya adui vya kutumia mabomu ya kusaga miamba dhidi ya maghala ya silaha ya Iran. Kwa mujibu wa wataalamu katika uga wa uhandisi wa vita, miji ya chini ya ardhi imejengwa kwa namna ambayo mabomu ya kupasua miamba hayawezi kupenya katika miji hiyo na kutoa pigo kwa uwezo wa silaha za Iran.
Kwa hivyo, kujenga miji ya makombora ya chini ya ardhi ni njia bora ya kuongeza nguvu za kujilinda na kumfanya adui asithubutu kuanzisha mashambulio.
Nukta ya mwisho ni kwamba, kuzinduliwa mafanikio muhimu ya kijeshi ya Iran kunaweza kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuwa na taathira madhubuti katika kuunda milinganyo mingi ya baadaye ya kisiasa na kistratijia katika ngazi ya kieneo. Lililo dhahir shahir ni kwamba, mafanikio haya ni kinyume kabisa na propaganda za adui kuhusu kudhoofisha nafasi ya kieneo ya Iran.