Iran na Iraq katika mkondo wa kuongeza maelewano na ushirikiano wa pamoja
Rais wa Iran amesema kuwa nchi za Kiislamu zinapasa kujiepusha na masuala yanayozusha hitilafu na badala yake zinapasa kushikama na kuwa kitu kimoja; na kwa njia hiyo ni wazi kuwa njama za maadui na wale wanaozitakia mabaya wenzao hazitafanikiwa.
Rais Masoud Pezeshkian amesema kushirikiana, maelewano na kuimarisha umoja miongoni mwa nchi za Kiislamu ni miongoni mwa mahitaji muhimu ya hali ya sasa ya dunia. Rais wa Iran amesema hayo hapa Tehran katika mazungumzo na Mahmoud al Mash'hadani Spika wa Bunge la Iraq na ujumbe anaoongozana nao ziarani hapa nchini.
Kadhalika Daktari Pezeshkian ameashiria matukio ya karibuni katika eneo hasa huko Syria na kusema: 'Msimamo wa Iran ni kuona Syria inaunda serikali jumuishi kwa kuyashirikisha makundi yote ya wananchi, inalinda umoja wa ardhi ya nchi hiyo na inazuia kugawanywa vipande nchi hiyo.'
Rais wa Iran pia amepongeza msimamo madhubuti na wa wazi wa Iraq katika kuwahami wananchi madhulumu wa Palestina na kusema, katika uga wa kuisaidia Gaza na Lebanon tunapendekeza kuwa nchi zote za Kiislamu kwa kadiri ya uwezo wao ziwasaidie watu wa maeneo hayo katika ujenzi mpya na kurejea katika makazi yao.
Katika mazungumzo hayo, Spika wa Bunge la Iraq pia ameeleza kufurahishwa na ziara yake nchini Iran na mazungumzo aliyofanya na viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hii na kusisitiza jitihada za Bunge la Iraq za kuiunga mkono serikali ya nchi hiyo katika kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi mbili.
Mahmoud al-Mash'hadani amesema Iraq inasisitiza kuimarisha ushirikiano wa pande mbili, wa kikanda na kimataifa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mohammed Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia alikutana na kufanya mazungumzo na Mahmoud Al-Mash'hadani, Spika mpya wa Bunge la Iraq. Ghalibaf amesema katika mazungumzo hayo kwamba, Iran na Iraq zina nafasi muhimu katika kuleta na kuimarisha usalama na utulivu katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Spika Qalibaf ameongeza kuwa: Licha ya hasara iliyopata kambi ya muqawama lakini ilisimama imara dhidi ya wingi huu wa suhula na zana za kijeshi na kuufanya utawala wa Kizayuni wa Israel ushindwe kufikia malengo yake.
Qalibaf aliendelea kusisitiza kuwa, hapana shaka kwamba Marekani na utawala wa Kizayuni ndio vinara wa njama katika ulimwengu wa Kiislamu na kusisitiza kuwa: Katika mazingiira kama haya ni lazima tuzuie hitilafu zozote za kikaumu na kidini.
Akizungumzia wasiwasi wa pamoja wa nchi hizo mbili, Mahmoud Al-Mash'hadani Spika wa Bunge la Iraq alisema katika mazungumzo yake na Spika wa Bunge la Iran kuwa nchi hizo mbili zinapaswa kuandaa mikakati mwafaka ili kuleta utulivu na kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi.
Safari ya Spika wa Bunge la Iraq mjini Tehran ni duru mpya ya mashauriano kati ya viongozi wa ngazi za juu wa Tehran na Baghdad na shabaha yake kuu ni kuimarisha na kupanua uhusiano wa pande mbili katika nyuga mbalimbali za kiuchumi, kisiasa, kiusalama na kiutamaduni.
Iran na Iraq ni nchi mbili jirani ambazo zina fursa mwafaka za ushirikiano wa pande mbili, na katika miaka ya hivi karibuni, licha ya mashinikizo na vizuizi vyote vya Marekani vya kukwamisha kuendelezwa uhusiano wa Tehran na Baghdad, mamlaka za nchi hizi mbili daima zimekuwa zikitaka kuoanisha misimamo ya kieneo na kupanua uhusiano wa pande mbili.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq ni wanachama muhimu wa Jumuiya ya Nchi Zinazouza Nje Mafuta kwa Wingi (OPEC) na zikiwa na akiba kubwa ya nishati na maeneo ya pamoja ya mafuta na gesi, zina msingi mzuri wa ushirikiano katika soko la nishati la kieneo na kimataifa.
Maadhimisho ya Tasua na Ashura ya Imam Hussein katika mwezi wa Muharram na Arubaini ya Imam Hussein katika mwezi wa Safar, kwa ajili ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Husein (AS) na masahaba zake watiifu, hufanyika kila mwaka huko Karbala Iraq na idadi kubwa ya watu hushiriki.
Katika miaka ya hivi karibuni, matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein yamepata nafasi ya pekee na yamekaribishwa duniani kote. Kumbukumbu hii ya kipekee na adhimu na mahudhurio makubwa ya mamilioni ya maashiki na vipenzi wa Imam Hussein ni mambo ambayo yameongeza ushirikiano kati ya mamlaka za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq.
Viongozi wa Iran na Iraq pia wana maoni yanayofanana kuhusu matukio ya kikanda na nafasi yenye ushawishi ya makundi ya muqawama. Kuzingatia na kutetea haki halali za wananchi wa Palestina; na kukabiliana na kiburi na upendaji makuu wa Marekani na utawala wa Kizayuni ni fursa mwafaka ya duru mpya ya ushirikiano kati ya Tehran na Baghdad.