Araghchi: Iran inaaminika, siku zote huheshimu kile inachosaini
Apr 22, 2025 10:50 UTC
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu Iran amesisitiza kuwepo hakikisho la kudhaminiwa maslahi ya kiuchumi ya Iran kupitia makubaliano yoyote yatakayofikiwa na akaeleza kuwa, Iran ni ya kuaminika na daima huheshimu kile inachotia saini.
Sayyid Abbas Araqchi, ametoa waraka wa hotuba yake ambayo alikuwa aisome kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Sera ya Nyuklia wa Carnegie, huko Washington na kueleza kwamba: "wapangaji sera wanaohusika, wanaelewa vyema kwamba kujitenga na mazungumzo na kujiingiza kwenye makabiliano kutachangia zaidi kuporomoka mkataba wa kuzuia uenezaji silaha za nyuklia kuliko kusaidia kuulinda".
Araghchi amebainisha kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa ni mmoja wa waasisi wa Mkataba wa NPT katika miaka ya 1960, daima imekuwa ikiheshimu misingi na kanuni zinazoruhusu nchi zote kunufaika na teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani na kupinga umiliki wa silaha za atomiki, na ndiyo nchi pekee ambayo imetangaza rasmi upinzani wake dhidi ya silaha za nyuklia kwa kuzingatia sababu za kimaadili na kidini, na kwamba kupingwa suala hilo kumebainishwa kwa fatua ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu inayoharamisha umiliki wa silaha za aina hiyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameendelea kueleza kwamba, kwa kufumbia macho maghala ya silaha za nyuklia za Israel na kupuuza hatua yake ya kukataa kujiunga na NPT au kukubali silaha zake kuwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, nchi za Magharibi zimeutia doa mkataba wa kimataifa wa kuzuia uenezaji silaha za nyuklia kupitia misimamo yao ya kindumakuwili.
Araghchi ameongezea kwa kusema: "sasa hivi ni mwaka 2025 na inapasa vipimo hivi vya undumakuwili vihitimishwe. Juhudi za Iran za kunufaika na nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani, zingali ndio vipaumbele vyake vya muda mrefu vinavyoendana na malengo ya kimaendeleo na kiuchumi ya nchi".../