Umuhimu wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran nchini China
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i125534-umuhimu_wa_ziara_ya_waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_iran_nchini_china
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amewasili Beijing leo (Jumatano), Aprili 23, kwa ajili ya kukutana na kufanya mashauriano na viongozi wa China.
(last modified 2025-04-23T10:03:32+00:00 )
Apr 23, 2025 10:03 UTC
  • Umuhimu wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran nchini China

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amewasili Beijing leo (Jumatano), Aprili 23, kwa ajili ya kukutana na kufanya mashauriano na viongozi wa China.

Mara baada ya kuwasili Beijing, Sayyid Araghchi amekaribishwa na maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China pamoja na Balozi wa Iran nchini humo, Mohsen Bakhtiar. Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran mjini Beijing imefanyika ndani ya kalibu ya kuimarisha ushirikiano wa kiistratijia kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na China na mashauriano ya ngazi za juu kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizi mbili.

Katika safari yake hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekwenda na barua kutoka kwa Rais Masoud Pezzekian wa Iran aliyomwandikia Rais mwenzake wa China, Xi Jinping.

Nchi mbili za Iran na China zina uhusiano mzuri

 

Kuhusu ziara ya Araghchi mjini Beijing, Guo Jiaqun msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema: "Ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran nchini China itakuwa na umuhimu mkubwa hasa katika kutekeleza makubaliano muhimu yaliyofikiwa na wakuu wa nchi hizo mbili, kuzidisha kuaminiana kisiasa kati ya pande hizi mbili, kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali na kutia nguvu ushirikiano wa pande nyingi."

Kwa upande wake, Ismail Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametuma ujumbe kwenye Mtandao wa X kuhusiana na ziara ya Araqchi nchini China na kuandika: "Iran na China, zina mtazamo wa pamoja katika masuala mengi ya kimataifa na zinakamilishana na kuheshimiana kama ambavyo pia zinachukua hatua za dhati za kuhakikisha zinalinda maslahi ya pande mbili." Aidha ameandika: "Mashauriano ya mara kwa mara na ya karibu kati ya pande hizi mbili katika ngazi za juu ni ishara tosha ya azma ya viongozi wa nchi mbili ya kupanua uhusiano katika nyanja zote zenye manufaa kwa mataifa yote mawili."

Araqchi, ambaye ameelekea Beijing kwa mwaliko rasmi wa waziri mwenzake wa China, amesisitizia umuhimu wa kustawishwa ushirikiano wa pande mbili na pande nyingi ikiwa ni pamoja na ndani ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na kundi la BRICS.

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

 

Mbali na kubadilishana mawazo na kufanya mashauriano kuhusu masuala yenye maslahi kwa pande zote mbili, Araqchi alikuwa na ratiba ya kujadiliana pia na viongozi wa China kuhusu mchakato wa utekelezaji wa mpango wa ushirikiano wa miaka 25.

China ni moja ya pande zenye maamuzi ya kujitegemea na ina nafasi nzuri katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran. Hivyo moja ya ajenda za mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na viongozi wa China ni suala la haki ya Iran ya kustafidi na matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.

Iran na China zilitia saini makubaliano ya ushirikiano wa miaka 25 mwaka 2021; na nchi hizo mbili, zikiwa wanachama muhimu wa kundi la BRICS na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, zinafanya jitihada za kuimarisha ushirikiano na kuwa na nafasi athirifu kwenye mifumo ya kiuchumi ya pande nyingi, matumizi ya sarafu mbadala ambazo si dola ya Marekani na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kikanda.

Misimamo na maslahi ya pamoja yamezifanya Iran na China kuwa washirika wawili wanaoaminiana na wanaoendeleza ushirikiano wao hata katika mazingira magumu sana. Hivi sasa kuimarishwa ushirikiano wa pande hizi mbili kuna umuhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote. 

Weledi wa mambo wanasema kuwa ziara ya Araqchi nchini China itakuwa na athari nzuri katika uhusiano wa kikanda na kimataifa kwani Iran na China zina nafasi muhimu katika milingano ya kimataifa na kikanda.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na China kupitia jumuiya mbili muhimu za kundi la BRICS ambalo ni muungano wa nchi zinazoinukia kiuchumi na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, zina nafasi kubwa katika ustawi wa uchumi wa dunia na kuimarisha usalama wa kieneo na kimataifa.

Bila ya shaka yoyote, kustawi ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na China kutakuwa na athari nzuri na kubwa pia katika masoko ya Asia Magharibi na Asia ya Kati hadi kwenye eneo la Eurasia. Iran, ni moja ya vitovu vya nishati duniani huku China ikiongoza katika uzalishaji wa bidhaa, mambo ambayo ni misingi bora ya kuongeza ushirikiano wa kiuchumi.