Leo ni siku ya maombolezo nchini kufuatia mripuko uliotokea katika Bandari ya Shahidi Rajaee
(last modified Mon, 28 Apr 2025 03:14:42 GMT )
Apr 28, 2025 03:14 UTC
  • Leo ni siku ya maombolezo nchini kufuatia mripuko uliotokea katika Bandari ya Shahidi Rajaee

Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa, leo Jumatatu ni siku ya maombolezo nchini kote kufuatia tukio la kusikitisha la mripuko uliotokea kwenye Bandari ya Shahid Rajaee iliyoko mjini Bandar Abbas, katika mkoa wa kusini wa Hormozgan.

Msemaji wa Serikali, Fatemeh Mohajerani, alitangaza hapo jana kuwa serikali imetangaza kuwa leo itakuwa siku ya maombolezo kote nchini kufuatia tukio hilo.
Aidha, Mohajerani ametoa salamu za pole na rambirambi kwa familia zilizofiwa na akasisitiza kuwa ufuatiliaji maalumu unafanyika kuhusiana na tukio hilo na kwamba Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Masoud Pezeshkian ameelekea mjini Bandar Abbas.
 
Rais Pezeshkian jana Jumapili mchana aliwasili Bandar Abbas makao makuu ya mkoa wa Hormozgan ili kufuatilia hali ilivyo hivi sasa katika tukio la mripuko uliotokea katika Bandari ya Shahid Rajaee na kusimamia kwa karibu masuala mbalimbali yanayohusiana na tukio hilo.
 
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran atahudhuria kikao cha dharura cha Tume ya Kushughulikia Majanga ya Mkoa, kinachofanyika kwa kushirikisha mawaziri na maafisa husika, ili mbali na kusikiliza ripoti za kinachoendelea kwenye eneo la tukio, kutoa maagizo muhimu ya kuharakisha ushughulikiaji wa hali zawaathirika, kufidia hasara na uharibifu, na kurejesha shughuli za Bandari ya Shahidi Rajaee katika hali ya kawaida.
 
Mripuko mkubwa ulitokea mwendo wa saa sita mchana siku ya Jumamosi katika bandari ya Shahidi Rajaee ambao chanzo chake hasa bado hakijajulikana.
 
Nguvu ya mripuko huo iliharibu baadhi ya majengo na magari yaliyokuwepo karibu na eneo la tukio.
 
Kwa niaba ya Rais, Waziri wa Mambo ya Ndani Eskandar Momeni na Waziri wa Barabara na Maendeleo ya Miji Farzaneh Sadeq walikuwepo eneo la tukio kuanzia saa za awali.
 
Pirhossein Kolivand, Mkuu wa Shirika la Hilali Nyekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza jana alasiri kwamba zaidi ya majeruhi elfu moja wa tukio la bandari ya Shahidi Rajaee wamefikishwa hospitalini na kabanisha kuwa, shughuli za utafutaji na uokoaji zimefanyika kwa ufanisi.
 
Kolivand alisema, majeruhi wengi wameruhusiwa kutoka hospitalini na akaongeza kuwa majeruhi 190 kwa sasa wangali wamelazwa hospitalini.
 
Mkuu wa Hilali Nyekundu ya Iran ameeleza pia kwamba, kwa masikitiko watu 28 wamefariki katika tukio hilo na wengine 20 wako kwenye kitengo cha wagonjwa mahututi.
 
Hadi sasa, nchi nyingi zikiwemo Belarus, Armenia, Russia, Saudi Arabia, Cuba, Venezuela, Bahrain, Uturuki, Oman, Iraq, Tajikistan, na Japan zimetuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika, pamoja na serikali na wananchi wa Iran.../