Haki ya Iran ya kurutubisha madini ya urani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza msimamo wa muda mrefu lakini wa kisheria wa Iran kuhusu kuwa na haki ya kurutubisha madini ya urani.
Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Araghchi amemwambia Antonio Guterres: Iran ikiwa ni mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) sambamba na kuzingatia wajibu wake, inasisitiza juu ya kunufaika kwake na nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani ambapo ili kufikia hilo ni lazima kurutubisha madini ya urani.
Aidha katika mazungumzo hayo, Araghchi amemfahamisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na mwenendo wa mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana baina ya Iran na Marekani na hatua zilizopigwa katika mazungumzo hayo.
Matamshi ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na haki ya Iran ya kuwa na mzunguko kamili wa fueli ya nyuklia na kurutubisha madini ya urani si msimamo wa kisiasa tu; bali, ni tafsiri ya kanuni za sheria za kimataifa na maandiko ya wazi ya ibara ya 4 ya NPT, ambayo inatambua haki ya nchi wanachama kumilikii teknolojia ya amani ya nyuklia, bila ubaguzi.

Iran ni mwanachama mwanzilishi na mtiaji saini mkataba huu mwaka 1968. Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) una mihimili mitatu ya msingi: Upokonyaji silaha, kutoeneza silaha, na matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia. Kifungu cha 4 cha mkataba huo kinasema kwa uwazi na bila utata kwamba, hakuna chochote katika mkataba kitakachofasiriwa kuwa kinapoteza na kukanyaga "haki ya asili ya nchi wanachama kwa ajili ya kuendeleza utafiti, uzalishaji na matumizi ya nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani."
Kwa kutumia kipengee hicho, Iran inadai haki zilezile ambazo nchi kama Ujerumani, Japan, Brazil na Uholanzi zimenufaika nazo kwa miaka mingi. Kwa mujibu wa taarifa rasmi na ripoti nyingi za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Iran sio tu kwamba imefanya shughuli zake chini ya usimamizi endelevu wa shirika hilo, lakini pia hakuna ushahidi wowote wa maana na madhubuti unaoonyesha kuwa mpango huo umekengeukka malengo ya amani na kuelekezwa kwenye malengo ya kijeshi.
Hata ripoti ya hivi karibuni zaidi ya Mkurugenzi Mkuu wa IAEA inaendelea kutangaza shughuli za nyuklia za Iran kwamba, zinafanyika chini ya usimamizi kamili wa wakala huo na hazijakengeuka mkondo wa amani. Licha ya uangalizi mkali zaidi wa mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, Marekani kwa mara nyingine inafuata sera ya mashinikizo ya juu zaidi ili kuinyima Iran haki hii inayotambuliwa kisheria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio hivi karibuni alisema kwamba Iran lazima "iachane kabisa na urutubishaji madini ya urani"; dai ambalo halina msingi wa kisheria katika NPT na ni onyesho tu la mtazamo wa kibabe. Wataalamu huru na taasisi za kimataifa zimesisitiza mara kwa mara uhalali wa kisheria wa kurutubisha madini ya urani kwa njia ya amani chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.
Kwa mfano, Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika hilo, Mohamed El-Baradei alisema: “Tukiiambia nchi ambayo ni mwanachama wa NPT kwamba isirutubishe madini ya urani, huku nchi zingine zikifanya hivyo bila mashinikizo, tunakuwa tumekiuka kanuni ya kutobagua katika mkataba huo.
Hans Blix, mtu mashuhuri katika uga wa sheria za nyuklia, pia anatoa hoja akisema kwamba urutubishaji si ukiukaji wa mkataba wenyewe, bali kuondoka katika mkondo wa amani ndio sababu ya wasiwasi, na katika kesi ya Iran, hakujawa na ushahidi wa kuthibitisha kwamba, Iran imekengeuka mkondo wa amani.
Licha ya kutilia mkazo juu ya kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani, Jamhuri ya Kiislamu iliingia katika mazungumzo ya muda mrefu ili kupunguza mvutano katika uhusiano wake na nchi za Magharibi, ambao hatimaye ulipelekea kutiwa saini makubaliano kati ya Iran na kundi la 5+1 mwaka 2015.
Lakini Trump aliiondoa nchi yake ya Marekani katika makubaliano haya katika utawala wake wa kwanza mnamo 2018 kwa kisingizio cha uwongo. Rais wa Marekani aliiwekea Iran vikwazo vya kidhalimu. Uzoefu wa kihistoria wa Iran wa kushirikiana na nchi za Magharibi umejaa ukiukaji ahadi na kutoaminiana. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Araqchi amesisitiza kuwa kuendeleza diplomasia kunahitaji dhamira ya dhati kwa upande wa pili na kuepuka kutoa "matakwa yasiyo ya kisheria."

Kujitoa kwa upande mmoja katika makubaliano ya nyuklia (JCPOA), kuweka na kuendeleza vikwazo na mashinikizo makali ya kiuchumi, na vitisho vya mara kwa mara vya kijeshi na kisiasa ni hatua ambazo zimechukuliwa na Marekani katika miaka ya hivi karibuni. Katika mazingira kama haya, kutarajia Tehran utekeleze matakwa ambayo ni zaidi ya majukumu ya mkataba sio tu kwamba ni jambo lisilowezekana, lakini pia ni kuonyesha utendaji wa kibaguzi na kutumia asasi za kimataifa kama wenzo wa kushinikiza mataifa mengine.
Nukta muhimu zaidi ni kuwa, ikiwa nchi ambayo imefuata na kutekeleza kikamilifu makataba wa NPT itanyimwa haki zake za kiufundi na kisheria, huko kutakuwa ni kutuma ujumbe hatari kwa nchi nyingine ambao ni: Kuwa mwanachama katika mkataba huo hakudhamini usalama wa kisheria na madola makubwa yana uwezo wa kufafanua upya masharti ya mikataba kwa mashinikizo ya kisiasa.
Hili ndilo onyo haswa ambalo limetolewa na wachambuzi huru, akiwemo Mark Hibbs wa taasisi ya Carnegie ya kwamba "mfumo wa kutoeneza silaha za nyuklia, utakuwa na faida pale tu wanachama wote watakapokuwa na hisia sawa na kuheshimi haki za wote”.
Ni kwa mtazamo huu, ndio maana Iran imekuwa ikitaka kudhaminiwa haki za kiufundi, kuondolewa vikwazo, na kuandaliwa mazingira ya manufaa halisi ya kiuchumi kupitia makubaliano hayo na si sio upendaji makuu.
Kwa muktadha huo, makubaliano yoyote mapya yanaweza tu kuwa endelevu na ya kutegemewa ikiwa yanategemea haki sawa, na kuheshimiana na si undumakuwili, ubaguzi na ubabe.