Si gereza Israel ni makaburi, ukitoka hai ndio ushangae
(last modified Sat, 10 May 2025 06:56:54 GMT )
May 10, 2025 06:56 UTC
  • Si gereza Israel ni makaburi, ukitoka hai ndio ushangae

Askari mmoja wa akiba wa jeshi la Israel ambaye wakati fulani alikuweko kwenye jela ya kutisha ya Israel ya Sde Teiman katika Jangwa la Negev amefichua taarifa za kutisha na kuogofya mno kuhusu jinai wanazofanyiwa Wapalestina kwenye gereza hilo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, askari huyo ameliambia gazeti la Haaretz kwamba jela ya Sde Teiman, iliyoko umbali wa kilomita 30 kusini mwa mji wa Be'er al Sab'i (Be'er Sheva), ni kambi ya mateso ya kutisha mno.

Askari huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema: "Baadhi ya Wapalestina wanaingia kwenye jela hiyo wakiwa hai lakini wanatoka maiti zao zikiwa zimebebwa kwenye mifuko." 

Amesisitiza kuwa, vifo vya mateka wa Palestina katika jela hiyo si jambo la kushangaza hata kidogo, bali cha kushangaza sana ni kuona Mpalestina anatoka akiwa hai kwenye gereza hilo. 

Eneo la gereza la kutisha la Sde Teiman la utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Vilevile mwanajeshi huyo wa Israel amesema kuwa, mateso na ukiukwaji wa haki za wafungwa unafanyika kwa utaratibu maalumu na kwa amri ya serikali ya Israel. Amesema: "Nilishuhudia majeruhi wa vita wakiwekwa kwenye jela hii kwa wiki kadhaa, wakiwa na njaa na bila ya matibabu yoyote."

Aidha amesema kuwa, mateka wa Kipalestina wanashikiliwa katika mazingira ya kinyama mno kwenye jela hiyo ya Israel na amemnukuu kamanda wa kambi hiyo akisema: "jela ya Sde Teiman ni makaburi."

Gazeti la Haaretz pia limemnukuu askari huyo wa Israel akisema kuwa, walinzi wa jela ya Sde Teiman hawaruhusu mateka wa Palestina kutumia vyoo licha ya kwamba mateka wengi katika gereza hilo ni raia wa kawaida na hawakuwahi kubeba silaha hata mara moja.