Watu 200 wafariki dunia kwa janga la mafuriko Nigeria
(last modified Wed, 04 Jun 2025 05:51:56 GMT )
Jun 04, 2025 05:51 UTC
  • Watu 200 wafariki dunia kwa janga la mafuriko Nigeria

Mafuriko makubwa yaliyotokea kaskazini mwa Nigeria wiki iliyopita yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 200.

Kamishna wa masuala ya kibinadamu wa jimbo la Niger Ahmad Suleiman ameziambia duru za habari kuhusiana na jana hilo na kueleza kwamba, mamia ya watu wengine hawajulikani walipo, na kuna wasiwasi kwamba wamefariki.

Amesema bado wanaendelea kuwatafuta wahanga hao, ingawa hawana uhakika wa kuwapata. Mji wa Mokwa ulikumbwa na mafuriko mabaya zaidi siku ya Alhamisi kutokana na mvua zilizonyesha usiku kucha, huku zaidi ya nyumba 250 zikiharibiwa na mafuriko.

Mabadiliko ya hali ya hewa yametajwa kusababisha hali hiyo nchini Nigeria, ingawa wakaazi wa Mokwa wamesema sababu za kibinadamu pia zimechangia.

Mji wa Mokwa ni kiungo kikuu cha kibiashara kati ya wafanyabiashara wa kusini na wazalishaji wa mazao ya kilimo wa kaskazini mwa Nigeria. Kwa kuzingatia hayo tutaona kuwa, madhara ya mafuriko hayo kwa binadamu na kwa uchumi ni makubwa sana.

Wakala wa Taifa wa Kusimamia Mambo ya Dharura nchini Nigeria (NEMA) uliitisha mkutano wa washikadau Ijumaa katika Jimbo la Niger ili kushughulikia maafa hayo na kujiandaa mapema ili kupunguza madhara kwa wananchi. Kampeni hiyo imepewa jina la "Kuimarisha Ustahimilivu, Kuimarisha Maandalizi," na imewaleta pamoja maafisa wa usimamizi wa maafa na washirika wao ili kuweka mikakati ya muda mrefu ya kukabiliana na mafuriko ya mara kwa mara. Rais Bola Tinubu wa Nigeria ameiamuru NEMA na vikosi vya usalama kuimarisha shughuli za kutafuta wahanga na uokoaji katika jamii zilizoathiriwa.