Waziri Mkuu mpya wa Sudan avunja serikali ya mpito
Waziri Mkuu mpya wa Sudan, Kamil Idris amevunja serikali ya mpito ya nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.
Shirika la habari la serikali SUNA liliripoti habari hiyo jana Jumapili jioni na kuthibitisha kuwa, Kamil Idris amevunja serikali ya muda ya nchi hiyo.
SUNA haikueleza ni lini serikali mpya, ya kwanza tangu vita vilipozuka kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF, itatangazwa.
Idris amechukua hatua hiyo, siku moja baada ya kula kiapo, mbele ya Abdel Fattah al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Mpito linalotawala nchini humo.
Waziri Mkuu mpya wa Sudan Kamil Idris alisema jana kwamba, vipaumbele vya serikali yake ni kurejesha usalama wa taifa na mamlaka ya serikali, miongoni mwa mengine.
Katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa la Sudan iliyorushwa na runinga ya serikali, Idris pia alisisitiza haja ya ufufuaji wa misingi ya kitaifa, mazungumzo jumuishi yatakayoongozwa na Sudan, na kukabiliwa kwa ubaguzi wa kikanda na ubaguzi wa rangi.
Nafasi ya Waziri Mkuu ilikuwa imesalia wazi tangu kujiuzulu kwa Abdalla Hamdok Januari 2022, kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Burhan Oktoba 2021.
Hamdok na viongozi wengine wa kiraia walizuiliwa kwa muda kabla ya kurejeshwa chini ya mpango wa kugawana madaraka kwa muda mfupi.