Tanzania: Tundu Lissu afikishwa Mahakamani chini ya ulinzi mkali
Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu imesikilizwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku upande wa serikali ukiendelea kuleta hoja kuwa bado upelelezi haujakamilika.
Mwenyekiti huyo wa Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania alifikishwa katika viunga vya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi. Magari mawili, yaliyosheheni askari wenye silaha, mbwa, walionekana mahakamani hapo. Kisha Lissu akaingizwa katika chumba namba 1 cha mahakama ambako nako kulisheheni jopo la mawakili wanaomtetea Lisu na mawakili wa upande wa Jamhuri.
Alipopandishwa katika chumba namba 1 cha mahakama tayari wka kesi yake kusikilizwa, Lissu, alinyoonyosha mkono na kuonyesha alama ya vidole viwili, ambayo ni kauli mbiu ya chadema. Kisha akawasalimia watu kadhaa waliohudhuria mahakamani hapo kwa kuwapa mikono. Kabla ya kesi kuanza, wafuasi wa Chadema waliokuwamo mahakamani hapo pamoja na Lissu walitamka neno ‘no reform, no election’ jambo ambalo lilimuinua Wakili wa serikali, Nasoro Katuga.
“Kwa sababu upelelezi wa shauri hili bado unaendelea baada ya jalada kupelekwa ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka kusomwa na kuona bado kuna mapungufu machache ya kumalizia,” alisema Katunga.
Mchuano wa mawakiili hao ulianza ambapo upande wa Serikali ya Tanzania uliieleza mahakama kuwa upelelezi bado haujakamilika. Hata hivyo upande wa mshtakiwa, Wakili Jeremiah Mtobesya aliambia mahakama iwasilishe upelelezi dhidi ya Lisu kwani mteja wake kuwa huru ni kwa maslahi mapana ya umma.
“Tunaomba mahakama hii ione hivyo kwamba ni ucheleweshaji usioweza kuvumilika. Nimekumbushwa na wenzangu hapa kuwa kwa kuwa mtuhumiwa ana kesi mbili, mbona ile nyingine upelelezi umekamilika,” alisema Mtobesya.
Hata hivyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga aliutaka upande wa jamhuri kutaja hatua kesi hiyo ilipofikia.