Jeshi la Nigeria laua magaidi 20 kaskazini mwa nchi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i127132-jeshi_la_nigeria_laua_magaidi_20_kaskazini_mwa_nchi
Takriban magaidi 20 wameuawa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na jeshi la Nigeria katika jimbo la kaskazini la Zamfara mwishoni mwa juma.
(last modified 2025-06-03T07:03:20+00:00 )
Jun 03, 2025 07:03 UTC
  • Jeshi la Nigeria laua magaidi 20 kaskazini mwa nchi

Takriban magaidi 20 wameuawa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na jeshi la Nigeria katika jimbo la kaskazini la Zamfara mwishoni mwa juma.

Ehimen Ejodame, msemaji wa Jeshi la Anga la Nigeria, amesema katika taarifa iliyotolewa jana huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria kwamba, zaidi ya pikipiki 21 za watu wanaoshukiwa kuwa magaidi ziliharibiwa wakati wa mashambulizi ya anga katika eneo la Maru la jimbo la Zamfara, siku ya Jumamosi.

"Operesheni hiyo ililenga kuzima shambulio kubwa lililopangwa kufanywa dhidi ya watu wa jamii zilizoko hatarini," imesema taarifa hiyo ikibainisha kuwa, taarifa za kijasusi zilizopokelewa na jeshi zilionyesha kuwa idadi kubwa ya wahalifu walikuwa wanajikusanya kwa wingi kwa nia ya kujiandaa kushambulia makazi ya raia.

Taarifa zaidi za kiintelijensia zinaonesha kuwa magaidi hao wameua baadhi ya wakulima na kuwateka nyara idadi isiyojulikana ya raia wakiwemo wanawake na watoto wadogo.

Hali hiyo imelilazimisha jeshi kuingilia kati na kufanya mashambulizi dhidi ya wapanda pikipiki walioshukiwa kuwa ni magaidi.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, vikosi vya nchi kavu vya jeshi la Nigeria vilipelekwa haraka kwenye eneo hilo. Wanajeshi hao walithibitisha kufanyika uharibifu mkubwa katika uvamizi huo wa magaidi. 

"Juhudi zinaendelea za kuwasaka na kuwaokoa wanakijiji waliotekwa nyara ambao walipelekwa katika msitu ulioko karibu na eneo hilo," imesema sehemu nyingine ya taarifa ya jeshi la Nigeria.