Tanzania: Jamii ya kimataifa idhibiti vyanzo vya migogoro duniani
(last modified Wed, 04 Jun 2025 06:00:27 GMT )
Jun 04, 2025 06:00 UTC
  • Tanzania: Jamii ya kimataifa idhibiti vyanzo vya migogoro duniani

Tanzania imeiasa jamii ya kimataifa kuweka mikakati madhubuti ikiwemo kuwashirikisha wanawake katika masuala ya amani na usalama, ili kudhibiti migogoro ambayo vyanzo vyake vikuu ni ukabila, ubaguzi wa rangi, itikadi kali na migogoro kuhusu maliasili na mipaka.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama uliofanyika jijjini Prishtina nchini Kosovo kuanzia Juni 2 hadi jana.

Waziri Kombo amesema kuwa, ili kuwa na dunia yenye amani na utulivu, jumuiya ya jimataifa inatakiwa kushirikiana na nchi mbalimbali kutoa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa amani duniani na kushirikisha makundi ya wanawake na vijana katika mchakato wa amani ili kuepukana na migogoro mingi ambayo husababishwa na ukabila, itikadi kali za kisisasa na kidini, kugombea rasilimali kama madini na ubaguzi wa rangi.

Balozi Kombo ambaye alihutubia kama mzungumzaji mkuu wakati wa Jopo la majadilino kuhusu mada isemayo ‘Utangamano wa Amani katika Karne ya 21: Nini kinahitajika,’ amesema kuwa, katika karne hii ya sayansi na teknolojia wanawake wana nafasi na umuhimu mkubwa wa kushirikishwa katika masuala ya amani na usalama tangu ngazi ya familia hadi kimataifa kwani wao ndio wahanga wakuu wa migogoro na walezi wa familia hususan pale amani inapotoweka.

Washiriki wa Mkutano wa 3 wa Kimataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama jijjini Prishtina, Kosovo

Aidha, akizungumza kuhusu Tanzania, Waziri Kombo amesema kuwa nchi hiyo chini ya uongozi imara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kulipa suala la amani na usalama kipaumbele kwa kushiriki kikamilifu katika jitihada za utatuzi wa migogoro iliyopo katika kanda na duniani kote kwa njia za amani.

Mkutano wa Kimataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama ni jukwaa linalowaleta pamoja wadau wa kimataifa waliojitolea katika kuhakikisha kunakuwepo ushiriki madhubuti wa wanawake katika kuzuia migogoro, ujenzi wa amani na shughughli za urejeshaji baada ya migogoro.